1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

USAID na WFP zasitisha msaada wa chakula kwa jimbo la Tigray

4 Mei 2023

Shirika la misaada la Marekani USAID na la Umoja wa Mataifa la mpango chakula duniani WFP yametangaza kusitisha kupeleka msaada wa chakula katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia kutokana na madai ya wizi.

https://p.dw.com/p/4QuiR
Äthiopien Die Chefin von USAID  Samanta Power
Picha: Seyoum Getu/DW

Shirika la USAID limesema limesitisha mpango wa kupeleka msaada katika eneo la Tigray na wakati huo huo limeanzisha uchunguzi juu ya wizi wa chakula cha msaada katika eneo hilo. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP nchini Ethiopia limethibitisha kwamba limechukua hatua hiyohiyo. Shirika hilo liliwaambia washirika wake mnamo Aprili 20 kwamba limesitisha shughuli za kupeleka chakula katika jimbo la Tigray na kwamba shughuli hizo zitaanza tena pale litakapohakikisha kuwa misaada muhimu itawafikia walengwa na si vinginevyo.

Shehena za chakula cha msaada kwa jimbo la Tigray kutoka kwa Shirika la WFP.
Shehena za chakula cha msaada kwa jimbo la Tigray kutoka kwa Shirika la WFP.Picha: AP

Msimamizi wa USAID Samantha Power, amesema wamegundua kuwa msaada wa chakula, uliokusudiwa kwa watu wa Tigray wanaoteseka kwa njaa, uliporwa na kuuzwa kwenye soko la ndani na kwamba uchunguzi umeanzishwa kubaini ubadhirifu huo.

Soma:Mfumuko wa bei ´wakamua mifuko´ ya familia Ethiopia

Power katika taarifa yake, amesema kufuatia tathmini hiyo, shirika la USAID, kwa ushirikiano na Ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa na washirika wake wameamua kusitisha kwa muda kupeleka msaada wa chakula katika jimbo la Tigray na kwamba wamewasilisha malalamiko kwa serikali ya shirikisho ya Ethiopia pamoja na kwa mamlaka ya jimbo la Tigray. Haijulikani ni nani aliyehusika na wizi huo wa chakula cha msaada na ni kiasi gani kilichochukuliwa mpaka sasa.

Takriban watu milioni 6 wa Tigray wanategemea msaada wa chakula, baada ya eneo hilo kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka miwili na vikwazo vilivyowekwa na serikali kuu kuhusu misaada ya kibinadamu jambo ambalo lilisababisha eneo hilo kutumbukia kwenye baa la njaa.

Ofisi za WFP nchini Ethiopia.
Ofisi za WFP nchini Ethiopia.Picha: Million Hailesilassie/DW

Mwezi uliopita, shirika la habari la AP liliripoti juu ya kutoweka vifaa pamoja na chakula cha kutosha kulisha watu 100,000, kilichotoweka kutoka kwenye ghala la mji wa Sheraro kwenye jimbo la Tigray. Kiongozi wa mpito wa jimbo la Tigray, amesema ameunda kikosi kazi cha kuchunguza matukio yanayohusiana na kuibiwa misaada ya kibinadamu na ameiamrisha kamati hiyo kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.

Marekani ndiyo mfadhili mkubwa wa misaada ya kibinadamu inayotolewa kwa Ethiopia. Kulingana na shirika la USAID Marekani ilitoa dola bilioni 1.8 kwa Ethiopia katika mwaka wa fedha wa 2022, kwa ajili ya misaada ya chakula. Mbali na vita vya wenyewe kwa wenyewe, Ethiopia vilevile inapambana na ukame wa muda mrefu.

Vyanzo:AP/AFP