Serikali ya Kenya yakabiliwa na rushwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Kenya yakabiliwa na rushwa

Masilahi ya kisiasa na kibinafsi yawekwa mbele

Waziri mkuu Raila Odinga, (kushoto) akisalimiana na rais Mwai Kibaki (katikati) huku makamu wa rais Kalonzo Musyoka akiwatazama

Waziri mkuu Raila Odinga, (kushoto) akisalimiana na rais Mwai Kibaki (katikati) huku makamu wa rais Kalonzo Musyoka akiwatazama

Makubaliano baina ya vyama vya PNU na ODM kuunda serikali ya muungano baada ya ghasia zilizotokana na uchaguzi Desemba 2007 yalitoa matumaini makubwa nchini Kenya. Hata hivyo ingawa pande zinazohusika zimeonyesha moyo mwema kutokana na hatua hiyo pamoja na nia ya kufanya kazi pamoja, lakini bado si kazi rahisi.

Tatizo kubwa ni watu kuweka mbele masilahi yao ya kisiasa na kibinafsi. Ama moja wapo ya changa moto kubwa ya serikali hiyo ya muungano ni Kukithiri kwa rushwa, jambo linalozidisha pengo katika serikali hiyo baina ya PNU na ODM.

Biashara kubwa kadhaa za siri kwa kiu cha kutaka kutajirika na hasa kuhusiana na usambazaji mahindi na Petroli, ni janga lililotokeza likizidi kuwanyonya wakenya. Kuzorota kwa uchumi duniani mwaka jana kulisababisha kushuka kwa bei ya mafuata kutoka dola 147 kwa pipa mwezi Julai hadi dola 40 katika nusu ya mwaka jana 2008.

Matokeo yake ni kwamba kampuni ya mafuta ya Trion, moja wapo ya zile zilizohusishwa katika kinyanganyiro cha biashara ya mafuta, ilijaribu kubakia katika bei ya juu, na hivyo kuwanyima Wakenya nafasi ya kufaidika na kupungua kwa bei.Hali hiyo ikasababisha uhaba usiotarajiwa wa mafuta katika kipindi cha Krismasi na kuzusha mshituko na wasi wasi katika masoko.

Uhaba wa mahindi uliosababisha kupanda bei zao hilo pia uliripotiwa nchini humo katika kipindi cha mwishoni mawa mwaka jana, na hali bado haijawa nzuri. Kinachosumbua katika masuala yote mawili-chakula na uhaba wa mafuta nchini Kenya, ni shutuma ya kwamba wanasiasa maarufu wamehusika wakishirikiana katika biashara hiyo na wafanya biashara wakubwa wakiwanyonya watu wa kawaida.

Wakenya wameachwa katika hali ya mshangao panapohusika na kiwango cha rushwa nchini kinachohatarisha usambazaji wa mahitaji muhimu, kama chakula na mafuta ya petroli. Katika sekta hizo mbili majina ya wanasiasa wanaotajwa hadharani ni kutoka vyama vyote, PNU na ODM. Kiraitu Murungi kutoka chama cha PNU ni waziri wa nishati na William Ruto wa ODM ni waziri wa kilimo. Kila mmoja anabebeshwa lawama, lakini hakuna aliyekubali kubeba jukumu. Kila mwanasiasa anapokumbwa na kashfa , wafuasi wake humlinda na kuutupia lawama upande wa pili.

Waziri Ruto anasema sababu ya uhaba wa mahindi ni ghasia za baada ya uchaguzi. Lakini waziri wa sheria na masuala ya katiba, Bibi Martha Karua, kutoka PNU anaripotiwa kuwalaumu maafisa katika wizara ya kilimo, akisema wanajinufaisha kutokana na uhaba wa mahindi. Katika upande wa viwanda, hali ni sawa na hiyo, huku Wakenya wakijikuta wanalipishwa Shilingi 85 kwa lita kutoka shilingi 75, licha ya kuwa bei ya mafuta sasa ni ya chini katika soko la dunia.

Kinachokosekana,wanasema wataalamu wa taasisi ya masuala ya usalama mjini Nairobi, kwamba ni uwajibikaji, utawala bora na uwazi ndani ya serikali ya muungano. Kwa hakika jukumu kubwa ni la watu wawili, Rais Mwai Kibaki wa PNU na Waziri mkuu Raila Odinga kutoka ODM.

Hadi sasa mawaziri Ruto na Murungi hawakutakiwa wajiuzulu na kusubiri matokeo ya uchunguzi. Ingawa huenda wanasubiri ripoti ya uchunguzi ya tume ya kupambana na rushwa nchini Kenya, KACC, lakini kwa bahati mbaya tume hiyo haina madaraka ya kumfungulia mtu mashitaka na hukabidhi tu ripoti yake kwa vyombo vya kisheria vichukuwe hatua. Ama uchunguzi huo unaweza ukaishia karatasini tu sawa na ilivyothihirika katika kashfa nyingi-kama ile ya Goldenberg au Angolo Leasing.

Wadadisi wanaonya kwamba bila ya wanasiasa kuchukua hatua zinazofaa kurudisha imani ya wananchi, kuendelea kwa hali ngumu inayowakabili wananchi wa kawaida, ni chachu ya mripuko wa kijamii.

 • Tarehe 28.01.2009
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohammed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gi4O
 • Tarehe 28.01.2009
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohammed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gi4O
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com