1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Serikali ya Israel yaponea kura ya imani

27 Machi 2023

Muungano wa wafanyakazi nchini Israel umeitisha mgomo mkuu leo kupinga mpango wa serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu wa kuifanyia mabadiliko idara ya mahakama.

https://p.dw.com/p/4PIkS
Israel Protest gegen die Justizreform
Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika siku moja baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kumuachisha kazi waziri wake wa ulinzi aliyekuwa ametaka usitishwaji wa mabadiliko hayo.

Katika ujumbe uliorushwa moja kwa moja kwenye televisheninchini Israel, mwenyekiti wa muungano huo wa wafanyakazi Histadrut, Arnon Bar-David, amesema lengo lao kuu ni kusitisha mchakato huo wa mabadiliko unaofanywa na serikali na kwamba watafanikiwa na hawatosita kupambana.

Mgomo baada ya kufutwa kazi kwa waziri

Chama cha Madaktari cha Israel nacho baada ya tangazo hilo, kimetangaza mgomo wake pia hatua itakayokuwa na athari katika hospitali zote za umma na mfumo mzima wa afya nchini Israel.

Yoav Gallant | israelischer Verteidigungsminister
Waziri wa ulinzi aliyeachishwa kazi Yoav GallantPicha: Gil Cohen-Magen/AFP/Getty Images

Mgomo huo wa nchi nzima umeitishwa saa chache baada ya Rais wa Israel Isaac Herzog kushinikiza kusitishwa mara moja kwa mpango huo wa mabadiliko unaopigiwa debe na serikalii, kauli yake ikiwa imejiri baada ya maandamano makubwa kufanyika Tel Aviv usiku kucha, waandamanaji wakiwa wanapinga kuachishwa kazi kwa waziri wa ulinzi Yoav Gallant.

Gallant ambaye pia ni mwandani wa Netanyahu, awali alikuwa ametaka kusitishwa kwa mchakato huo wa mageuzi. Muda mchache uliopita serikali ya Netanyahu imeponea chupuchupu katika kura iliyopigwa bungeni juu ya imani kwa serikali hiyo.

Kiongozi wa upinzani Yair Lapid naye ametoa wito wa kuachana na mchakato huo wa mageuzi.

"Hatustahili kuanguka na kuvunjika, kuna suluhisho. Natoa wito kwa serikali ya muungano, twendeni katika makao ya rais na tuanze mazungumzo ya kitaifa na mwishowe tutakuwa na katiba yenye msingi wa azimio la uhuru na nchi ambayo sote tunaishi pamoja kwa kuheshimiana," alisema Lapid.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitarajiwa kulihutubiataifa baadae leo huku kukiwa na uvumi katika vyombo vya habari nchini Israel kwamba atasitisha mageuzi hayo anayoyafanya katika idara ya mahakama. Hata hivyo hotuba hiyo imeahirishwa.

Marekani yataka maafikiano

Hatua ya kutaka kuweka udhibiti zaidi kwa wanasiasa na kuipoteza kabisa dhima ya Mahakama ya Juu ni jambo lililosababisha maandamano yaliyodumu kwa miezi kadhaa nchini Israel na kumekuwa na hofu hata miongoni mwa marafiki wa Israel ikiwemo Marekani.

Israel Protest gegen Justizreform in Jerusalem
Waandamanaji katika mitaa ya JerusalemPicha: Ammar Awad/REUTERS

Marekani imetoa wito wa maafikiano  huku ikulu ya White House ikisema Rais Joe Biden hivi majuzi alimwambia Waziri Mkuu Netanyahu kwamba uhusiano wa nchi zao mbili unastahili kusalia katika misingi ya kidemokrasia.

Serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Netanyahu inasema mageuzi hayo yanahitajika ili kuleta usawa wa nguvu kati ya wabunge na idara ya mahakama.

Hapo jana waandamanaji walikusanyika nje ya makao ya waziri mkuu huku wengine wakiandamana katika mji wa kaskazini wa Haifa na wa kusini wa Beer Sheva.

Chanzo: DPAE/AFPE/APE