1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seehofer: Bundesliga irejee mwezi huu

4 Mei 2020

Waziri wa mambo ya ndani na michezo Ujerumani Horst Seehofer amesema anaunga mkono kuendelea kwa msimu wa kandanda mwezi huu licha ya kuwa kumegunduliwa maambukizi mapya ya virusi vya corona katika klabu ya FC Cologne.

https://p.dw.com/p/3blHO
Horst Seehofer (CSU) Bundesminister für Inneres
Picha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Usimamizi wa ligi kuu ya Ujerumani DFL unaunga mkono pia kuanza tena kuchezwa kwa mechi katikati ya mwezi huu wa Mei ila bila mashabiki uwanjani. Hatua hii itaifanya Bundesliga kuwa ligi ya kwanza kuu Ulaya kurejea uwanjani.

Seehofer lakini amesema vilabu na wachezaji ni sharti wafuate sheria zitakazowekwa ila ameongeza kwamba vilabu havitapendelewa katika suala la upimaji wa virusi kwani kanuni zitakazotumika ni zile zile zitakazotumika kwa ajili ya kuwapima watu wengine wote Ujerumani. Baadhi ya vilabu vilikuwa vimetaka wachezaji wake wapimwe mara kwa mara.

Mashabiki ni sehemu yetu wachezaji

Vilabu vya Ujerumani tayari vinaendelea na mazoezi kujiweka tayari endapo tangazo la kuendelea kwa mechi litatolewa wakati wowote. Alphonso Davies ni beki wa shoto wa mabingwa watetezi Bayern Munich na hapa anatoa maoni yake kuhusiana na mechi kuchezwa bila mashabiki uwanjani.

UEFA Champions League | FC Chelsea - Bayern München
Beki wa shoto wa Bayern Munich Alphonso DaviesPicha: picture-alliance/Newscom/P. Terry

"Ikifanyika hivyo itakuwa tofauti kabisa. Mashabiki ni sehemu yetu ila ni kwa ajili ya usalama wa kila mmoja nafikiri, kwa hiyo mimi sitojali sana kucheza bila mashabiki. Nafikiri kwa sasa kila mmoja analenga kusalia kuwa mwenye afya uwanjani na nje ya uwanja pia," alisema Davies.

Nchini Ufaransa Paris Saint Germain tayari walitangazwa mabingwa baada ya Waziri Mkuu wa Ufaransa Edouarde Philippe kutangaza hakutokuwa na michezo yoyote nchini humo hadi Septemba.