1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yakata mahusiano na Canada

Isaac Gamba
8 Agosti 2018

Saudi Arabia imekata mahusiano ya kiuchumi na  Canada na kumfukuza balozi wake kufuatia wito wa Canada kuitaka imuachie mwanaharakati wa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/32o2r
Mohammed bin Salman
Picha: picture-alliance

Jumatatu wiki hii Saudi Arabia ilimpa  saa 24 balozi wa Canada nchini humo Dennis Horak kuondoka nchini humo na kutangaza  ni mtu asiyetakiwa kabisa katika taifa hilo huku pia ikitangaza kuwa mahusiano yote mapya ya kibiashara kati yake na Canada yatasitishwa.

Hatua hiyo inafuatia ujumbe  kupitia ukurasa wa twitter ulioandikwa wiki iliyopita na waziri wa mambo ya nje wa Canada Chrystia Freeland akisema Canada  ina wasiwasi mkubwa  na kuendelea kutiwa mbaroni wanaharakati wa haki za binadamu  na za wanawake nchini Saudi Arabia  akiwemo Samar  Badawi ambapo Freeland alitoa mwito kwa serikali ya Saudi Arabia kuwaachia huru haraka.

Saudi Arabia  imekosoa ujumbe huo kupitia ukurasa wa twitter ikisema unaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuwa unakiuka sheria za taifa hilo la Kifalme na pia mfumo wake wa kimahakama.

Aidha Saudi Arabia imesema itazuia maelfu ya wanafunzi wa nchi hiyo kwenda kusoma Canada huku shirika la ndege la nchi hiyo likitangaza kusitisha safari zake kwenda Canada kuanzia August 13.

Mataifa kadhaa ya kiarabu katika ukanda huo yameonesha kuunga mkono  hatua ya Saudi Arabia dhidi ya Canada huku Anwar Gargash waziri wa  mambo ya nje katika Umoja wa Falme za Kiarabu akisema wataendelea kuiunga mkono Saudi Arabia katika kulinda mamlaka yake.

Kwa upande wake Mohammad bin Abdullah al-Zulfi mchambuzi wa masuala ya kisiasa  na mjumbe wazamani wa baraza la ushauri nchini humo alisema anaunga mkono  hatua iliyochukuliwa  na mwana wa mfalme Mohammad bin Salman pamoja na serikali yake dhidi ya Canada. Ameieleza DW kuwa  Saudi Arabia ni taifa kubwa na haihitaji Canada, Ujerumani au Marekani.

 

Marekami yasema hilo ni suala lakidiplomasia

USA Donald Trump zum Atomdeal mit Iran
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Reuters/J. Ernst

Hayo yanajiri huku  Marekani ikisema suala kati ya Saudi Arabia na Canada ni la kidiplomasia na litapaswa kutafutiwa ufumbuzi na nchi zote mbili.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umesema wanahitaji maelezo kuhusiana na hatua ya kukamatwa wanaharakati wa  haki za wanawake nchini Saudi Arabia.

Maja Kocijancic msemaji wa Umoja wa Ulaya  amesema wamekuwa wakiitaji ufafanuzi tangu Mei mwaka huu kutoka Saudi Arabia kuhusiana na hatua ya nchi hiyo kuwatia mbaroni wanaharakati kadhaa.

Amesema Umoja wa Ulaya unataka kufahamu vema kuhusiana na tuhuma  dhidi ya wanaharakati na kuhakikisha wanatendewa haki katika shauri lao.

Hii si mara ya kwanza Saudi Arabia kuingia katika mzozo wakidplomasia kuhusiana na suala la mwanaharakati Badawi kwani mwaka 2015 iliwahi kumuita balozi wake nchini Sweden baada ya waziri wa mambo ya nje wa Sweden kukosoa uamuzi wa mahakama kuhusiana na kesi ya mwanahakati huyo hatua iliyofuatiwa na kusimamisha viza za kazi nchini humo kwa raia wa Sweden.

Mwandishi: Isaac Gamba/DW/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga