1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya US juu ya nuklia, Iran yasema ni ushindi mkubwa kwao

Aboubakary Liongo6 Desemba 2007

Rais Mahmoud Ahmednejad amesema kuwa ripoti iliyotolewa na idara za ujasusi za Marekani juu ya mpango wake wa nuklia, ni ushindi mkubwa kwa nchi yake.

https://p.dw.com/p/CXis
Iran imeshinda katika mzozo juu ya mradi wake wa kinyuklia?Picha: AP

Rais huyo wa Iran amesema hayo kufuatia ripoti iliyotolewa na idara hizo hapo siku ya Jumatatu ikisema kuwa Iran ilisitisha mpango wa kutengeza silaha za nuklia toka mwaka 2003.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye mji wa Ilam Magharibi mwa Iran,Ahmednejad amesema kuwa ripoti hiyo ni pigo kubwa kwa wale ambao kwa miaka kadhaa wameigubika dunia kwa vitisho na shinikizo akimaanisha Marekani.

Amesema kuwa Marekani imeondoka patupu na wao wameibuka na ushindi mkubwa.

Hata hivyo Rais Ahmednejad akasema kuwa nchi hiyo iko tayari kuupokea mkono wa maridhiano lakini ukinyooshwa kwa upendo na urafiki na si mkono huo ukinyoosha kidole cha uadui.

Kwa ripoti hiyo kutolewa kiongozi huyo akaonya kuwa yoyote atakayetaka kuanzisha mzozo mpya na nchi hiyo wananchi wa Iran watajibu vikali na kamwe hawatarudi nyuma hata hatua moja.

Iran kwa sasa inakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa kutokana na kukaidi azimio linaloitaka kusitisha urutubishaji wa uranium ambao nchi hiyo imekuwa ikisisitiza kuwa nishati hiyo ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Mapema Rais George W Bush alisisitiza kuwa Iran bado ni tishio na akasema ni lazima itimize masharti ya Umoja wa Mataifa kabla ya kwenda katika meza ya majadiliano.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la kimataifa la Atomic Mohamed El Baradei akizungumza mjini Brasilia Brazil amesema kuwa ripoti hiyo kwa kiasi fulani imeisafisha Iran na kwamba inatoa nafasi mpya kwa wanadiplomasia kushughulikia suala hilo.

Naye mkuu wa zamani wa shirika hilo Hans Blix amesema kuwa ripoti hiyo ina maana kuwa hakutakuwa na hatua zozote za kijeshi dhidi ya Iran katika kutanzua mzozo huo.

Mjini Washington Makamu wa Rais wa Marekani Dicky Cheney amekiri kuwa ripoti hiyo inaweza kukwaza harakati za kidiplomasia za nchi hiyo katika suala la Iran.

Dickey Cheney anakuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu wa Marekani kukiri kuwa ripoti hiyo inaweza kuweka kiwingu katika juhudi za nchi hiyo kutaka Umoja wa Mataifa kuongeza zaidi vikwazo dhidi ya Iran iwapo itaendelea kukaidi azimio la kuitaka kusitisha urutubishaji wa nishati ya uranium ambayo ni malighafi muhimu katika kutengeza bomu la nuklia.

Akiwa ziarani nchini Ethiopea Waziri wa Nje wa Marekani Condoleza Rice alisema kuwa utawala wa Iran unabakia kuwa hatari na tatizo kwa dunia.

Ujerumani, Ufaransa na Uingereza mbali ya kutolewa kwa ripoti hiyo zimeleeza kuunga kwao mkono hatua zaidi dhidi ya Iran iwapo itaendelea na ukaidi wake.

Lakini China na Urusi baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo zimekuwa kimya katika kuungana na Marekani kutaka kupitishwa kwa azimio lingine na Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Iran.

Urusi imetaka kutiliwa maanani kwa ripoti hiyo kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kuiwekea vikwazo Iran na kusema kuwa hata idara yake ya ujasusi haina ushahidi kuwa Iran ilikuwa na mpango wa kutengeza bomu la nuklia kabla ya mwaka 2003.