Rex Tillerson aanza ziara Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rex Tillerson aanza ziara Afrika

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson anatarajiwa kuwasili nchini Ethiopia mchana wa leo (07.03.2018), nchi hiyo ikiwa kituo chake cha kwanza katika ziara itakayomfikisha katika nchi tano za bara la Afrika.

Mexiko NAFTA-Verhandlungen | Rex Tillerson (Reuters/H. Romero)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson

Ziara ya Rex Tillerson inafanyika wakati uhusiano kati ya Marekani na China ukighubikwa na wingu la matamshi ya Rais Donald Trump mwanzoni mwa mwaka huu, aliyezilinganisha nchi za Afrika na mahali penye uvundo.

Kabla ya kuondoka mjini Washington, Rex Tillerson ambaye ndiye afisa wa ngazi ya juu wa Marekani kuizuru Afrika tangu utawala wa Rais Donald Trump ulipoingia madarakani zaidi ya mwaka mmoja uliopita, amesema Marekani inaichukulia Afrika kama bara lenye Mustakabali mwema, na kwamba ingependa kushiriki katika mchakato wa kujenga ustawi wa watu wa bara hilo.

Mwanadiplomasia huyo anabeba jukumu la kufafanua sera ya Trump kuhusu Afrika, kwa sababu mbali na kutoa matamshi ya kuzikashifu nchi za bara hilo, viongozi wengi wa kiafrika hawana habari kuhusu anavyowachukulia.

Kupambana na ushawishi wa China

Lakini pia ziara hiyo ya Tillerson inafanyika wakati China ikizidi kujiimarisha barani Afrika kwa kasi ambayo inaitia wasiwasi Marekani. Wachambuzi wanasema kudhibiti ushawishi wa China katika mataifa ya Afrika ni miongoni mwa agenda kuu za ziara hii ya Tillerson. Katika kuonyesha tofauti ya kimtazamo baina ya nchi yake na China kuhusu Afrika, Tillerson amesema Marekani inalenga kuisaidia Afrika kujijengea uwezo wake yenyewe.

Mali Bamako - Brückenbau (picture-alliance/Photoshot)

China imeimarisha ushawishi wake barani Afrika kupitia biashara na ujenzi wa miundombinu

Amesema, ''Marekani inafuata njia ya maendeleo endelevu, kwa kuimarisha taasisi na utawala wa sheria, na inazijengea nchi za Afrika uwezo wa kujisimamia zenyewe.'' Tillerson ameongeza kuwa Marekani inashirikiana na nchi za Kiafrika kuendeleza utawala bora kwa lengo la kutimiza malengo ya maendeleo ya muda mrefu.

''Hii ni tofauti kabisa na China ambayo inataka Afrika iendelee kuitegemea, kwa kusaini mikataba isiyo ya uwazi, kutoa mikopo migumu, na kupenyeza mtindo wa biashara ambao utazifanya nchi za Afrika kuzama katika mgogoro wa madeni.'' Amesema waziri huyo wa Marekani.

Msaada wa Marekani kwa Afrika

Tillerson vile vile amepigia debe msaada wa Marekani kwa Afrika, akikumbushia kusainiwa mwezi Septemba mwaka jana kwa mpango wa PEPFAR, wenye lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI barani Afrika kati ya mwaka 2017 na 2020. Nchi 50 za Kiafrika zinanufaika na mpango huo.

Karte Eritrea Djibouti DEU (DW)

Marekani na China zote zina maslahi ya kijeshi katika taifa dogo la Djibouti

Ziara ya Tillerson ya takriban wiki moja barani Afrika itamfikisha pia katika mataifa ya Kenya, Djibouti, Naigeria na Chad. Changamoto za kiusalama na za ugaidi zitapewa kipaumbele katika mazungumzo na viongozi wa mataifa hayo.

Nchi ya Djibouti ina maslahi ya kipekee kwa Marekani, kwa sababu licha ya kuwa kituo cha makao makuu ya jeshi la Marekani barani Afrika, nchi hiyo ndogo ya Upembe wa Afrika pia imeiruhusu China kujenga kituo chake cha kijeshi, cha kwanza nje ya China.

Ingawa hii ni ziara ya kwanza ya Rex Tillerson barani Afrika akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, yeye si mgeni katika bara hilo. Aliwahi kuzitembelea nchi kadhaa akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni kubwa ya mafuta ya Exxon Mobil, katika safari za kibiashara, akifika Chad, Nigeria na Guinea ya Ikweta.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, rtre

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com