Rais Wulff ahimiza mafungamano baina ya Wajerumani na Waturuki | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Wulff ahimiza mafungamano baina ya Wajerumani na Waturuki

Rais wa Ujerumani Christian Wulff yuko kwenye ziara ya siku tano nchini Uturuki, ambapo leo hii (19.10)amepewa heshima ya kulihutubia bunge la nchi hiyo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Ujerumani kufanya hivyo.

Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Christian Wulff (kushoto) na mwenyeji wake Rais Abdullah Gül wa Uturuki

Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Christian Wulff (kushoto) na mwenyeji wake Rais Abdullah Gül wa Uturuki

Rais Christian Wulff amewahimiza Waturuki na Wajerumani kuangalia yale mengi yanayowaunganisha kuliko yale machache yanayowatenganisha, kwani watu wa nchi hizi mbili ni marafiki wa siku nyingi.

"Mambo haya yanayotufungamanisha ni ya thamani zaidi kuliko utengano wetu, maana katika utengano ndimo tunamojikuta tunagombana, kwa mfano, kwa kuendekeza hamasa zetu na ufahamu wetu mbaya wa dini badala ya kufuata misingi halisi ya dini hizo." Amesema Rais Wulff.

Kauli hii inakuja katika wakati ambapo hapa Ujerumani, mjadala wa kuwajumuisha Waislam wapatao milioni nne katika jamii ya Kijerumani unaendelea. Wengi wa Waislam hao ni Waturuki. Mapema mwezi huu, Rais Wulff aliwashangaza Wajerumani wengi, pale aliposema kwamba, kama palivyo kwa Ukristo na Uyahudi, Ujerumani pia ni nyumbani pa Uislam.

Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Christian Wulff (kulia) akipokea heshima ya kijeshi akiwa na mwenyeji wake Rais Abdullah Gül wa Jamhuri ya Uturuki, kwenye makaazi ya rais mjini Ankara, Jumanne ya 19 Oktoba 2010. (Picha na Rainer Jensen, DPA)

Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Christian Wulff (kulia) akipokea heshima ya kijeshi akiwa na mwenyeji wake Rais Abdullah Gül wa Jamhuri ya Uturuki, kwenye makaazi ya rais mjini Ankara, Jumanne ya 19 Oktoba 2010. (Picha na Rainer Jensen, DPA)

Kwenye mahojiano yake yaliyochapishwa leo (19 Oktoba 2010) na gazeti la kila siku la Hurriyet la Uturuki, Rais Wulff amesema kwamba ni jambo la lazima kwa wahamiaji kujifunza Kijerumani ili waweze kujijumuisha na jamii ya Kijerumani kwa mafanikio, lakini amelipinga wazo la Waziri Mkuu mhafidhina wa jimbo la Bavaria, Horst Seehofer, ambaye alipendekeza kwamba Ujerumani izuie kuwajumuisha Waislam kwenye jamii.

"Kujifunza Kijerumani tu ndiko kunakoweza kufungua milango yote kwa mfumo wa elimu. Lakini nafikiri si sawa kusema kwamba kundi zima la watu haliwezi au halitaki kujijumuisha na wenzao." Amesema Rais Wulff.

Suala la Waturuki kujifunza Kijerumani linaungwa mkono pia na Rais wa Uturuki, Abadallah Gul, ambaye amesema kwamba, badala ya watu kulitumia suala la kujumuishwa kama tatizo la kisiasa, wanapaswa kusaidia kutafuta suluhisho kwa kujifunza lugha ya wenyeji wao.

Lakini katika kuchangia mjadala huu, Kansela Angela Merkel, alisema hivi karibuni kwamba, uwezekano wa tamaduni tafauti kuchanganyika na kuishi pamoja hapa Ujerumani ni jambo ambalo limefeli kabisa. Akiwa amekabiliwa na mkururo wa chaguzi ngumu hapo mwakani, Kansela Merkel alisema kwamba ile dhana ya Multikulti inayosema kwamba Wajerumani wanaweza kuishi bega kwa bega na wageni haifanyi kazi.

"Sisi Wajerumani tumejifungamanisha na hulka za Kikristo. Wale ambao hawakubaliani na hulka hizo, hawana nafasi hapa." Alisema Kansela Merkel.

Wiki ijayo, baraza la mawaziri la Kansela Merkel litapitisha hatua madhubuti kuhusiana na uhamiaji, kulazimisha mafunzo ya lugha ya Kijerumani kwa wageni na kupambana na ndoa za kulazimishwa.

Ziara ya Rais Wulff inatarajiwa pia kuzungumzia suala la uwanachama wa Uturuki kwenye Umoja wa Ulaya, ingawa msimamo wa Ujerumani ni kwamba nchi hiyo haiwezi kuwa mwanachama. Kansela Merkel akiwa na msimamo sawa na Rais Nicolas Sarkuzy wa Ufaransa, amesema kwamba Uturuki haina nafasi katika Umoja wa Ulaya na kwamba kitu pekee inachoweza kupigania ni ushirikiano na sio uwanachama kamili. Pendekezo hili linakataliwa na serikali ya Uturuki.

Mapema leo (19.10) asubuhi, Rais Wulff alitembelea makumbusho maalum ya mwanzilishi wa dola ya sasa ya Kituruki, Mustapha Kemal Ataturk. Anatarajiwa pia kulihutubia jukwaa la wafanyabiashara wa Uturuki na Ujerumani na kuhudhuria huduma ya kidini katika kanisa kongwe la Mtakatifu Paulo katika mji wa Tarsus kabla ya kushiriki kwenye ufunguzi wa Chuo Kikuu cha Ujerumani na Uturuki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

 • Tarehe 20.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PhzH
 • Tarehe 20.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PhzH
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com