Rais wa Mali ajiuzulu baada ya kukamatwa na wanajeshi waasi | Matukio ya Afrika | DW | 18.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais wa Mali ajiuzulu baada ya kukamatwa na wanajeshi waasi

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ametangaza kujiuzulu kupitia televisheni, saa chache baada ya wanajeshi waasi kumkamata sambamba na Waziri wake mkuu Boubou Cisse katika mji mkuu wa Bamako.

Akizungumza kupitia kituo cha utangazaji cha taifa ORTM, Keita amesema kuwa kujiuzulu kwake kunaanza mara moja. Awali picha na vidio zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha msafara unaoaminika kuwa wa rais Keita na waziri mkuu Cisse uliokuwa umezingirwa na wanajeshi. Kukamatwa kwa viongozi hao kuna litumbukiza taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na makundi ya wanajihadi na maandamano katika mgogoro mkubwa.

Picha na vidio zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha msafara unaoaminika kuwa wa rais Keita na waziri mkuu Cisse uliokuwa umezingirwa na wanajeshi, waliokuwa wakitembea bila woga kwenye mitaa ya Bamako. Kiongozi mmoja wa waasi aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina amesema kuwa "rais na waziri mkuu wako chini ya udhibiti wetu, baada ya kukamatwa katika makazi ya Keita mjini Bamako". Soma zaidi Wanajeshi wajaribu kuasi Mali, milio ya risasi nje ya kambi

Afisa mmoja wa jeshi Sidi Gakao amethibitisha taarifa hizo alipozungumza na shirika la habari la DPA kwa njia ya simu akisema kwamba "rais na waziri wake mkuu wamekamatwa".

Mali I Soldaten nehmen nach Meuterei Präsident und Regierungschef fest (Getty Images/J. Kalapo)

Wanajeshi wa Mali wakipita mitaani

Wanajeshi walianza uasi huo mapema siku ya Jumanne katika mji wa Kati, uliopo kilometa 15 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Bamako ambapo milio ya risasi ilisikika. Taarifa za kukamatwa viongozi wa serikali zilipokelewa kwa furaha na umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katikati ya mji kwa ajili ya kushinikiza Keita kujizulu.

Jumuiya ya kimataifa yalaani jaribio la mapinduzi

Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika zote zimelaani uasi huo na kuonya juu ya jaribio lolote la kubadili madaraka kinyume na katiba katika taifa hilo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka "kuachiwa haraka na bila masharti" kwa rais Keita na Cisse wakati wanadiplomasia mjini New York wakisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura hii leo kwa ajili ya kujadili hali nchini Mali.

Kauli kama hiyo ya kutaka Keita kuachiwa pia imetolewa na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat. ECOWAS kwenye taarifa yake, imewataka wanajeshi kurejea kwenye kambi na kujizuia dhidi ya "kitendo chochote kinyume na katiba" na kujaribu kutatua tofauti za kisiasa kupitia mazungumzo.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umesema "unalaani jaribio la mapinduzi nchini Mali na unakataa mabadiliko yasiyo ya kikatiba". Taarifa hiyo imeongeza kwamba hatua hiyo haiwezi kuwa suluhisho la mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao umeikumba Mali kwa miezi kadhaa. Soma zaidi Rais wa Mali na Waziri Mkuu wakamatwa na wanajeshi waasi

Paris Mali PM Boubou Cisse 2019 (picture-alliance/AP Photo/F. Mori)

Waziri Mkuu wa Mali Boubou Cisse

Ufaransa ambayo iliitawala Mali nayo imekemea uasi huo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa kwenye taarifa yake imesema "inalaani tukio hilo kwa nguvu zote". Balozi za Marekani, Australia na Sweden mjini Bamako zilikuwa zimewaonya raia wake kubakia majumbani kufuatia ghasia zilizokuwa zikiendelea.

Mapema siku ya Jumanne, serikali ya Mali ilitoa taarifa ya kutaka utulivu na kusema iko tayari kwa mazungumzo. Mali imekuwa ikijaribu kurejesha utulivu tangu maelfu ya wafuasi wa upinzani walipoingia barabarani wakimtuhumu Keita kwa ufisadi na kudhoofika kwa usalama katika eneo la kaskazini na kati pamoja na udanganyifu katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Aprili. Lakini kampeni dhidi ya Keita iliongezeka mwezi uliopita baada ya watu 11 kuuwawa wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama, kufuatia maandamano ya siku tatu. Mazungumzo baina ya serikali na upinzani, yanayoongozwa na mhubiri maarufu Mahmoud Dicko, mshirika wa zamani wa Keita yaligonga mwamba.

Uasi kama huo ulifanyika kwenye kambi hiyo hiyo ya Kati mwaka 2012 na kusababisha mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais wa wakati huo Amadou Toumani Toure na kulifanya eneo la kaskazini kuangukia mikononi mwa wanamgambo. Kukosekana utulivu nchini mali kunatishia usalama wa kanda nzima ya Sahel, ambayo tayari inakabiliwa na vitisho kadhaa kutoka makundi ya kigaidi na wale wanaotaka kujitenga.

Vyanzo: AP/Reuters/AFP/DPA