Imam Dicko haoni haja ya Rais Keita wa Mali kujiuzulu | Matukio ya Afrika | DW | 30.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

MALI

Imam Dicko haoni haja ya Rais Keita wa Mali kujiuzulu

Kiongozi huyu wa Kiislamu anayeaminika kuunga mkono vuguvugu la maandamano nchini Mali anasema sasa mzozo wa kisiasa unaolikumba taifa hilo unaweza kutatuliwa bila ya Rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu.

Imam Mahmoud Dicko, ulamaa mwenye ushawishi mkubwa na ambaye amekuwa akiwaongoza waandamanaji licha ya mwenyewe kutokuwa mwanachama wa Vuguvugu la Juni 5, alionekana kuchukuwa msimamo wa wastani kwenye mahojiano yake na shirika la habari la Reuters siku ya Jumatano (Julai 29). 

"Nadhani tunaweza kupata suluhisho bila kufikia umbali wa rais kujiuzulu. Ukiwacha kujiuzulu kwake, kuna mengi yanayoweza kufanywa," alisema.

Alipoulizwa endapo ameridhika na kuondoshwa kwa aliyekuwa waziri mkuu, Boubou Cisse, ambaye amekuwa akilaumiwa vikali kwa jinsi alivyowashughulikia waandamanaji, Sheikh Dicko alisema mabadiliko hayo pekee hayawezi kuutatuwa mkwamo wa kisiasa uliopo, bali yanaweza kuwa sehemu ya muafaka.

Hotuba za Imam Dicko zilizoulaumu utawala wa Keita zimekuwa zikiwashajiisha sana waandamanaji, na washirika na mahasimu kwa pamoja wanamuona kama injini muhimu ya maandamano. 

Hata hivyo, baadhi ya washirika wa rais wanamuona kama ni  mtu aliye wazi kwa majadiliano na wanaamini kwamba maandamano yatapoteza nguvu bila ya yeye.

Mashaka ya mgawanyiko wa wapinzani

Licha ya kuwa na msimamo tafauti na viongozi wengine wa maandamano, Imam Dicko, ambaye kamwe hajawahi kumtaka Keita ajiuzulu, alikanusha kwamba kuna mgawanyiko ndani ya upinzani.

Mali Imam Mahmoud Dicko | Forderung nach Rücktritt von Präsident Ibrahim Boubacar Keita in Bamako (Reuters/M. Rosier)

Wafuasi wa Imam Mahmoud Dicko wakihudhuria maandamano dhidi ya Rais Ibrahim Boubacar Keita mjini Bamako.

"Hakuna mgawanyiko. Kuna vuguvugu moja tu ambalo wanademokrasia wanajuwa kuwa tafauti zao ndio nguvu zao," alisema kwenye mahojiano hayo na Reuters.

Maelfu ya waandamanaji wameingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge, ufisadi na ugoigoi serikalini. Mauaji ya waandamanaji 14 yaliyofanywa na polisi mwezi huu yamezidi tu kuchochea hasira za watu dhidi ya Keita.  

Licha ya Rais Keita kuridhia matakwa kadhaa ya waandamanaji na mapendekezo yao juu ya mageuzi yaliyotolewa na viongozi wa kikanda kutoka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, viongozi wa muungano wa upinzani wa M5-RFP wanaoratibu maandamano hayo, walisema juzi Jumanne kwamba wanamtaka Keita ajiuzulu na wakatowa wito wa maandamano zaidi dhidi yake.

Katika hatua nyengine, kundi la wabunge ambalo linalalamikiwa kuingia bungeni kupitia wizi wa kura na waandamanaji limekataa kujiuzulu kama ilivyopendekezwa na viongozi wa ECOWAS, hili likiwa ni pigo jengine kwa jitihada za jumuiya hiyo kuukwamuwa mkwamo wa kisiasa nchini Mali.

Kiongozi wa wabunge hao 31, Gougan Coulibaly, alisema kwamba hawatajiuzulu kwa kuwa "pendekezo hilo la ECOWAS linakwenda kinyume na katiba ya Mali." 

Tayari muungano wa upinzani ulishaukataa mpango wa usulihishi wa ECOWAS, lakini kukataa huku kwa wabunge wa chama cha Keita kujiuzulu kunaifanya hali kuwa mbaya na ngumu zaidi kwa wapatanishi hao.