Rais Magufuli aomba kura Mwanza | Matukio ya Afrika | DW | 07.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Magufuli aomba kura Mwanza

Mgombea wa Urais kupitia chama cha Mapinduzi Dr John Magufuli ameendelea na ziara ya kuomba Kura kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kwa kuhutubia mkutano Mkubwa wa Kampeni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akiwarai raia kumchagua tena, Rais Magufuli ameelezea yale aliyoyafanya katika kipindi cha miaka mitano na ahadi zake kama atachaguliwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akihutubia hadhira ya wakazi wa Mwanza na vitongoji vyake,Mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya CCM ambaye aliingia Mwanza hiyo jana akitokea Mkoani Mara,amewaambia wakazi wa Mwanza kuwa kama atapewa ridhaa ya miaka mitano mingine,atahakikisha anaiunganisha Mwanza katika sekta ya miundombinu ili kuifanya Mwanza iwe kitovu cha biashara kwa nchi za ukanda wa maziwa makuu na mikoa ya jirani.

Mgombea huyo wa Urais kupitia CCM,mbali na kuzungumzia ahadi za mwaka 2020 mpaka 2025 amegusia pia utekelezaji wa ahadi zake katika sekta ya usafiri hususani mkoa wa  Mwanza na ukanda wa ziwa Viktoria.

Ukanda wa Ziwa ni ukanda ulio na migodi mikubwa nchini Tanzania,sekta ambayo Mgombea wa Urais wa CCM John Magufuli mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015 alitupia jicho kwa kusitisha kwa muda uchimbaji wa madini ya dhahabu mpaka pale serikali na wawekezaji watakaaa pamoja, katika hotuba yake hii leo Magufuli amezungumzia kile ambacho serikali yake imefaidika.

Toka kuanza kwa kampeni hizi, hoja juu ya ajira, nyongeza ya mishahara na mahusiano ya kimataifa zimekuwa moja ya ajenda kubwa kwa baadhi ya wagombea.

Mgombea wa Urais wa CCM John Magufuli yupo kwenye ziara katika mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo tayari ameshafanya mikutano ya kampeni kwenye mikoa ya Dodoma,Singida, Shinyanga, Simiyu, Mara na leo amehutubia mkoani Mwanza na mara baada ya kukamilisha ziara ya Mwanza, ataelekea Mkoa wa Geita.