1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yakumbuka miaka 75 ya Ghetto la Warsaw

Sylvia Mwehozi
19 Aprili 2018

Wapoland na viongozi wa kiyahudi leo wameadhimisha miaka 75 ya vuguvugu la gheto la Warsaw lililofanywa na wayahudi waliokuwa wakizuiwa katika makambi na kisha kufanya uasi. 

https://p.dw.com/p/2wLNU
Polen 75. Jahrestag - Aufstand im Warschauer Ghetto Andrzej Duda
Picha: Reuters/K. Pempel

Rais wa Poland Andrzej Duda na kiongozi wa Umoja wa Wayahudi duniani rais Ronald Lauder, wamesema mamia ya vijana wa kiyahudi waliochukua silaha mjini Warsaw mnamo mwaka 1943 dhidi ya jeshi la kinazi la Ujerumani, walipigana kwa heshima lakini pia kuikomboa Poland kutoka mikononi mwa Wajerumani.

Uasi huo ulisabisha vifo vya karibu wapiganaji wote, na kuacha nyuma ishara ya kudumu ya upinzani. "Tunainamisha vichwa vyetu chini kwa ushajaa wao, ujasiri, na uamuzi wao", Duda aliwaambia mamia ya maafisa, waathirika wa mauaji ya wayahudi, Holocaust na wakazi wa mji wa Warsaw waliokusanyika siku ya Alhamis katika mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa uasi wa Warsaw.

Polen 75. Jahrestag - Aufstand im Warschauer Ghetto Andrzej Duda
Rais wa Poland Andrzej Duda wakati wa maadhimisho hayoPicha: Reuters/K. Pempel

"Waliangamia kwa sababu hiyo ndiyo iliyokuwa hatma ya wengi wao. Waliangamia wakipigana kwa heshima, wakipigana kwa ajili ya uhuru, lakini waliangamia na hizi ndizo hisia zetu, kupigana pia kwa ajili ya Poland kwa sababu walikuwa raia wa Poland", amesema Duda.

Kiongozi wa Umoja wa Wayahudi Ronald Lauder amesema kwamba wayahudi, Wapoland na watu wote wanapaswa kusimama pamoja kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo havipitii hofu kama ya mauaji ya Holocaust na vita ya Warsaw miaka 75 iliyopita.

Watu walisimama mitaani na maafisa walisimama wima wakisindikizwa na ving'ora na kengele za kanisa, majira ya mchana ili kuwakumbuka wayahudi waliopoteza maisha katika vuguvugu hilo, pamoja na mamilioni ya wayahudi wengine waliouawa katika mauaji ya wayahudi, Holocaust.

Utamaduni wa makaratasi ya njano ulianzishwa na Marek Edelman, kamanda wa mwisho aliyenusurika katika uasi huo, ambaye kila kumbukumbu alikuwa akiweka maua kwenye mnara wa kumbukumbu wa wapiganaji. Alifariki dunia mwaka 2009.

Katika sherehe nyingine kwenye ukumbi wa mji wa Warsaw, wahanga watatu wa Holocaust walitunukiwa uraia wa heshima wa mji huo.

Polen 75. Jahrestag - Aufstand im Warschauer Ghetto Andrzej Duda
Rais wa Umoja wa Wayahudi duniani Ronald LauderPicha: Reuters/K. Pempel

Asasi moja ya Open Republic ambayo inapambana na chuki dhidi ya wayahudi na chuki dhidi ya wageni, iliandaa sherehe tofauti na kile ilichokiita "mashimo mashuhuri ya kitaifa" na kukumbusha namna gani waziri mkuu mapema mwaka huu alipotoa heshima zake kwa kikundi cha wanamgambo wa Poland kilichoshirikiana na wanazi.

Mwaka huu, rekodi ya watu 2000 wa kujitolea walikuwa wakigawa makaratasi ya njano, ambayo yamekuwa alama ya wakristo wa Poland wanaoelezea huzuni zao kupoteza jumuiya ya kiyahudi iliyokuwa kubwa barani Ulaya kabla ya mauaji ya Holoaust.

Vuguvugu la Gheto la Warsaw liliibuka Aprili 19 mwaka 1943, wakati wapiganaji wadogo wa kiyahudi wapatao 750 walipojihami kwa bastola na chupa za mafuta na kuvamia jeshi kubwa lenye silaha nzito la Ujerumani. Wajerumani waliwaua karibu wapiganaji wote kasoro wachache waliofanikiwa kutoroka kupitia mifereji ya maji taka. Maadhimisho makubwa pia yamefanyika nchini Israel kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa taifa hilo mwaka 1948.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Josephat Charo