1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duda: Wanachama wa NATO waongeze bajeti ya kujihami

12 Machi 2024

Rais wa Poland Andrzej Duda amesema wanachama wa NATO wanapaswa kuongeza bajeti zao za kiulinzi hata kufikia asilimia tatu ya pato lake la ndani kwa shabaha ya kukabiliana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4dPWA
Polen Zeremonie Regierung Kabinett
Rais wa Poland Andrzej Duda akizungumza wakati wa hafla ya kumwapisha Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki na Baraza jipya la Mawaziri mjini Warsaw, Poland, Novemba 27, 2023.Picha: Czarek Sokolowski/dpa/picture alliance

Umoja huo kwa sasa una shabaha ya bajeti ya ulinzi ya asilimia mbili ya pato la ndani, ingawa Poland imevuka kiwango hicho na kufikia karibu karibu asilimia 4 ya pato lake.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya ziara yake kuelekea Washington na Brussels, Duda amesema anapendekeza katika siku zijazo, kukiondoa kile alichokiita kizingiti kwa kuwataka wanachama wa NATO waamue kwa pamoja kuwa mahitaji ya muungano yatatakiwa kutumia si asilimia mbili, bali asilimia tatu ya pato la taifa kwa ajili ya ulinzi.

Duda alisema NATO lazima itoe "jibu la wazi na la ujasiri" kuhusu unyanyasaji unaofanywa na Urusi. Katika hotuba yake kwa taifa, Duda ameliita pendekezo lake kuwa ni "jibu bora kwa vitisho dhidi ya usalama wa kimataifa" .Kiongozi huyo leo hii anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk na Rais wa Marekani Joe Biden kwenye maadhimisho ya miaka 25 tangu Poland, Jamhuri ya Czech na Hungary zilipojiunga na NATO.