Pakistan yaikasirisha Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Pakistan

Pakistan yaikasirisha Marekani

Mahakama kuu ya Pakistan imemwachia huru Ahmed Saeed Omar Sheikh aliyehukumiwa hapo awali baada ya kupatikana na hatia ya kupanga mauaji ya mwandishi wa habari wa Marekani Daniel Pearl mnamo mwaka 2002.

Msemaji wa ikulu ya Jen Psaki amesema Marekani imekasirishwa na uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Pakistan na amesisitiza kuwa Psaki amesema Marekani haikufurahishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Pakistan wa kumwachia huru Sheikh na watuhumiwa wengine watatu waliohusika na utekaji nyara na mauaji ya kinyama ya Daniel Pearl na kwamba hiyo ni dharau kwa wahanga wa ugaidi kila mahala ulimwenguni na ndani ya Pakistan. Msemaji huyo wa ikulu ya Marekani ameitaka serikali ya Pakistan kuangalia upya vipengee katika sheria zake pamoja na kuiruhusu Marekani imfungulie mashtaka Omar Sheikh kwa mauaji ya kinyama ya raia wa Marekani na mwandishi wa habari.

Mahakama Kuu ya Pakistan iliamuru kuachiwa huru kwa Mpakistani Ahmed Saeed Omar Sheikh mwenye uraia wa Uingereza pia ilitupilia mbali rufaa ya kupinga kuachiwa kwake iliyowasilishwa na familia ya Pearl pamoja na serikali ya Pakistan.

Ahmed Omar Saeed Sheikh mtuhumiwa wa mauaji ya mwandishi wa habari raia wa Marekani David Pearl.

Ahmed Omar Saeed Sheikh mtuhumiwa wa mauaji ya mwandishi wa habari raia wa Marekani David Pearl.

Waziri wa sheria wa jimbo la Sindh, Murtaza Wahab ambako Sheikh anashikiliwa amesema serikali imefuata taratibu zote ili mtu huyo aendelee kubakia kifungoni lakini haikufaulu na kwamba Sheikh anaweza kuwa huru tena katika siku chache zijazo. Amesema Mahakama Kuu ndio yenye mamlaka ya kutoa uamuzi wa mwisho nchini humo na tayari imefanya hivyo.

Familia ya Pearl kupitia kwa wakili wao Faisal Siddiqi imesema imeshtushwa mno na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Pakistan wa kumwachia huru Ahmad Omar Sheikh na watuhumiwa wengine watatu ambao wanaamini walimteka nyara na kumuua Daniel Pearl. Mahakama Kuu katika siku zijazo inatarajiwa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na uamuzi wake wa siku ya Alhamisi.

Kuuliwa kikatili kwa Pearl kuliwashtua wengi mnamo mwaka 2002, kabla ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu kuanza kuchapisha video za wanamgambo wake walioonekana wakiwaua kwa kuwakata vichwa waandishi wa habari waliokuwa wamewateka. Ripoti ya uchunguzi wa kifo chake ilisema Daniel Pearl, aliyekuwa mwandishi wa habari wa jarida la Wall Street alitolewa uhai wake kinyama.

Kushoto: Ahmed Saeed Sheikh baba yake Omar Saeed Sheikh mtuhumiwa wa mauaji ya Daniel Pearl. Kulia Mehmood A. Sheikh wakili wa familia ya Saeed Sheikh.

Kushoto: Ahmed Saeed Sheikh baba yake Omar Saeed Sheikh mtuhumiwa wa mauaji ya Daniel Pearl. Kulia Mehmood A. Sheikh wakili wa familia ya Saeed Sheikh.

Sheikh alihukumiwa kwa kusaidia kumhadaa Pearl kuhudhuria mkutano katika mji wa bandari wa Karachi, kusini mwa Pakistani ambako alitekwa nyara na kisha kuuawa. Pearl alikuwa akichunguza uhusiano kati ya wanamgambo wa Pakistan na bwana Richard C. Reid, aliyefahamika kwa jina la  "mshambuliaji aliyetumia viatu" baada ya mtu huyo kujaribu kuilipua ndege iliyokuwa inatoka mjini Paris, Ufaransa kwenda Miami, Marekani huku akiwa ameficha vifaa vya kulipuka katika viatu vyake.

Mwili wa Pearl uligunduliwa ukiwa umefukiwa kwenye kaburi lililokuwa la kina kifupi mara tu baada ya video ya kuuliwa kwake kupelekwa kwenye Ubalozi wa Marekani mjini Karachi. Idara ya ulinzi ya Marekani mnamo 2007 ilitoa nakala ambayo ilimwonesha Khalid Sheikh Mohammad, anayedaiwa kuwa ni kiongozi wa mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani aliyekiri kumuua Pearl.

Vyanzo:/AP/RTRE

 

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com