1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni za jeshi la Marekani nchini Syria zashutumiwa

Zainab Aziz
5 Juni 2018

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeishutumu Marekani na washirika wake kwa kutojali maisha ya raia wakati waliposhambulia mji wa Raqqa huko nchini Syria.

https://p.dw.com/p/2ywwe
Beitrag Journeyman The Ruins of Raqqa
Picha: Journeyman

Shirika la Amnesty International katika ripoti yake mpya limesema mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya kijeshi vilivyoongozwa na Marekani ya mwaka 2017 katika mji wa Raqqa yalisababisha vifo vya mamia ya raia pamoja na kuharibiwa vibaya mji huo ambapo baadhi ya sehemu zake ziligeuka kuwa maeneo yaliyojaa rundo la vifusi. Madai hayo hata hivyo yamekanushwa na jeshi la Marekani. 

Wachunguzi wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu waliwahoji wakazi zaidi ya 100 na pia waliyatembelea maeneo 42 yaliyoshambuliwa na vikosi hivyo vya muungano chini ya majeshi ya Marekani katika kipindi cha wiki mbili mnamo mwezi Februari walipokuwa wanafanya uchunguzi huo ambapo matokeo yake yamechapishwa katika ripoti iliyopewa jina la "Vita ya Uharibufu mkubwa," ikiwa ni marejeo ya lugha aliyoitumia waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis kwenye kampeni kabla ya operesheni hiyo.

Benjamin Walsby, mchunguzi wa masuala ya Mashariki ya Kati wa shirika la Amnesty International amesema kama watu wataendelea kuuwawa mara kwa mara kwenye operesheni za kijeshi basi bila shaka kuna matatizo.

Wakazi wa mji wa Raqqa wanajikongoja kurejesha maisha ya kawaida
Wakazi wa mji wa Raqqa wanajikongoja kurejesha maisha ya kawaidaPicha: DW/F. Warwick

Mji wa Raqqa wakati mmoja ulikuwa ni mji walikoishi takriban watu 200,000. Mji huo ulikumbwa na mashambulizi kwa zaidi ya miezi minne mnamo mwaka 2017, wakati ambapo muungano huo wa kijeshi ulioongozwa na majeshi ya Marekani ulipokuwa unaviunga mkono na kuvisaidia vikosi vya kijeshi vya Kikurdi (SDF). Muungano huo ulifanya mashambulio hayo hadi wanamgambo walipoondoka kutoka kwenye mji huo wa Raqqa mnamo mwezi Oktoba 2017.

Wakazi wa eneo hilo wamelalamika kuwa muungano huo wa kijeshi ulipiga mabomu kiholela bila kujali maslahi ya raia na hivyo wanadai fidia. Kulingana na Baraza la mji wa Raqqa asilimia 65 ya makazi ya watu ya meharibiwa.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo