Obama atoa ujumbe wa umoja Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama atoa ujumbe wa umoja Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani amewatolea wito Wamarekani wa tabaka zote kuwa na umoja na maelewano baada ya kuongezeka kwa uhasama kati ya maafisa wa usalama na watu weusi nchini humo.

Obama ameyasema hayo katika ibada ya kuwaombea askari watano waliouawa Dallas wiki iliyopita, huku akitarajiwa leo kukutana na wakuu wa polisi katika Ikulu ya Rais.

Akiwa ameambatana na mkewe, Michelle, kwenye ziara hiyo ya mjini Dallas, mji uliokumbwa na mkasa wa aina yake wa mshambuliaji mwenye asili ya Kiafrika kuwauwa askari Wamarekani wenye asili ya Kizungu, Obama amesema anaelewa kuwa Wamarekani wanasumbuliwa hivi sasa na kile ambacho wameshuhudia katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Mauaji ya Dallas yameongeza uhasama

Obama ameongeza kusema mfululizo wa matukio ya ufyatulianaji risasi yaliyochochewa na ubaguzi wa rangi yamepelekea kuwepo hisia kali zinazotilia shaka demokrasia nchini Marekani.

Askari akipita mbele ya picha za askari waliouawa Dallas

Askari akipita mbele ya picha za askari waliouawa Dallas

Hii leo, Rais Obama atajaribu tena kuwaonesha maafisa wa usalama kuwa yupo pamoja nao na anawaunga mkono na wakati huo huo, akijaribu pia kulizungumzia tatizo sugu la mahusiano kati ya askari na watu weusi, ambapo daima kumekuwa na malalamiko kuwa jamii hiyo ya Wamarekani inaangaliwa vibaya na vyombo vya dola.

Kikao cha leo katika Ikulu ya Rais mjini Washington kati ya Obama na maafisa wa usalama ni cha pili kufanyika katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Mkutano wa leo utawajumuisha pia mameya wa miji, wasomi na wanaharakati wa asasi za kiraia.

Katika ukurasa wake wa Facebook, rais huyo wa Marekani amesema watapata suluhisho kutoka kwa jamii ambazo tayari zimepata njia za kujenga imani na kupunguza tofauti miongoni mwao.

Obama na makamu wake, Joe Biden, siku ya Jumatatu walikutana na wawakilishi wa vyama vinane vya polisi kabla ya kuelekea Dallas hapo jana kuhudhuria ibada ya wafu ya askari watano waliouawa na mwanajeshi wa zamani wa Marekani, ambaye alisema alitaka kuwaua watu weupe hasa askari kutokana na jinsi wanavyowanyanyasa na kuwaua watu weusi.

Mauaji hayo ya Dallas yalitokea wiki iliyopita wakati wa maandamano ya amani ya kupinga mauaji ya wanaume wawili weusi waliouawa na askari weupe katika majimbo ya Louisiana na Minnesota.

Je ubaguzi wa rangi utapungua Marekani?

Obama amesema katika kusonga mbele kama taifa, anataka kusikia mawazo kutoka kwa Wamarekani zaidi kuhusu jinsi ya kushughulikia changamoto kwa pamoja kama taifa kwa kuwasilisha mawazo yao kupitia mtandao ulioanzishwa na serikali ili kupokea maoni ya raia.

Micah Xavier Johnson aliyewaua polisi watano Dallas

Micah Xavier Johnson aliyewaua polisi watano Dallas

Msemaji wa Ikulu ya Rais, Josh Ernest, amesema rais anatumai midahalo kuhusu namna ya kukabiliana na uhasama kati ya maafisa wa polisi na raia, yatafikia suluhisho madhubuti ambalo serikali na jamii zinaweza kulifanyia kazi.

Hata hivyo, kumekuwa na manung'uniko miongoni mwa polisi kuwa Rais Obama amekuwa mwepesi katika kuwashutumu polisi wakati matukio ya kuuawa kwa watu weusi yanapotokea.

Biden amesema baadhi ya vyama vya polisi vimeelezea wasiwasi wao kuhusu usalama wa wanachama wao na baadhi yao wameelezea kutofurahishwa na jinsi Rais anavyoshughulikia suala hilo la uhasama kati ya polisi na umma.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com