Obama atatangaza kikosi chake cha kushughulikia uchumi | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama atatangaza kikosi chake cha kushughulikia uchumi

Rais mteule wa Marekani, Barack Obama, anatarajiwa jumatatu kutangaza rasmi kikosi chake kitakachoshughulikia masuala ya kiuchumi.

Timothy Geithner

Timothy Geithner

Kikosi hicho kinakabiliwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na mgogoro wa kiuchumu mkali kuwahi kutokea katika historia ya uchumi wa nchi hiyo kwa kipindi cha miongo kadhaa iliopita.

Katika hatua inayoonekana kama kuanza mikakati ya kukabiliana na mzozo wa kifedha unaoikumba nchi yake,Obama pia anatazamiwa kufanya mkutano na waandishi habari.

Rais Mteule wa Marekani katika mkutano wa waandishi habari atakaouhutubia baadae jumatatu,atautumia kutangaza waziri wake wa fedha.

Chaguo lake inasemekana ni Timothy Geithner ambae ni mkuu wa Benki ya Akiba ya Marekani yenye makao yake mjini New York.

Chaguo la Geithner kama waziri mpya wa fedha ambalo liligusiwa siku ya Ijumaa lilisababisha kupanda kwa bei katika masoko ya hisa Dow Jones ambayo ilikuwa imeshuka wiki iliopita katika kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea tangu mwaka wa 1997.

Mshauri ya Obama David Axelrod amehakikisha chaguo la rais mteule Obama kuhusu nafasi ya waziri wa fedha.Mshauri huyo katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha Marekani mwishoni mwa juma amemuelezea waziri mypa kama mtu alie na ujuzi wa kutosha katika masuala ya kukabilina na migogoro ya kiuchumi,tangu alipokuwa naibu waziri wa fedha akihusika na mashauri ya kimataifa mika ya 90.

Ameongeza kuwa kutokana na nafasi yake kama rais wa benki ya akiba ya Marekani ya New York, afisa huyo ina maana amekuwa akihusika kwa njia moja ama nyingine na mgogoro wa sasa wa kifedha.

Rais Mteule pia anatarajiwa kumtangaza mjumbe mwingine katika kikosi chake kipya kitakachoshughulika na kufufua uchumi.Mtu huyo anajulikana kwa jina la Lawrence Summers.Anatazamiwa kuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya kiuchumi.Zamani alikuwa waziri wa fedha wakati wa utawala wa Bill Clinton.

Hata hivyo mshauri wa Obama Axelrod amekataa kuhakikisha uvumi eti Gavana wa New Mexico Richardson anaweza akateuliwa kama waziri wa masuala ya biashara.

Nafasi ya waziri wa fedha wa Marekani inachukuliwa kama nafasi moja muhimu nchini humo. Msimamo huo unazidi kupewa nguvu kutokana na kuwa sasa ofisi hiyo inajukumu la kusimamia donge la dola billioni 750 la kuzisaidia taasisi za kifedha za Marekani ambazo zinapata matatizo.

Na hayo yakiarifiwa mshauri wa rais mteule Obama ameonya kuwa kampuni tatu kubwa zinazotengeneza magari nchini humo ni lazima zije na mpango madhubuti ambao unaonyesha jinsi zinataraji kufanya kazi kabla ya baraza la Congress halijakubali fungu la kuyapiga jeki.

Makampuni hayo ya Ford,Chrysler na General Motors yameomba msaada wa pesa ,lakini wabunge wameyakatalia.

Afisa huyo amesema kuwa kampuni hizo ni lazima zibadili mikakati yake ya utenda kazi wakati ujao la sivyo walipa kodi hawakotaya kuyasaidia tena.

Kuhusu uvumi wa uwezekano wa kuteuliwa seneta Hillary Clinton kama waziri wa mashauri ya kigeni,mshauri huyo wa Obama amesema Bi Clinton ni mtu mwenye mwenye akili pamoja na uwezo.

 • Tarehe 24.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G1CB
 • Tarehe 24.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G1CB
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com