1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyadhfa za juu katika Umoja wa Ulaya bado zajadiliwa

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
1 Julai 2019

Hata baada ya kujadiliana usiku kucha viongozi wa Umoja wa Ulaya bado hawajakubaliana kuhusu warithi wa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker.

https://p.dw.com/p/3LOQn
EU-Gipfel in Brüssel | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: Reuters/Y. Herman

Hata baada ya kutumia muda wa saa 18 kujadiliana viongozi hao wa Umoja wa Ulaya bado hawajafikia makubaliano. Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanasema viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakaribia kufikia makubaliano juu ya baadhi ya nafasi za juu na Frans Timmermans wa chama cha Leba cha nchini Uholanzi anaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kuchukua nafasi ya Jean-Claude Juncker kama Rais mpya wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Hii ni kutokana na mkutano uliofanyika kandoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za G20 huko Japan wiki iliyopita.

Hata hivyo, pendekezo hilo limekutana na upinzani mkali kutoka nchi za Ulaya Mashariki pamoja na muungano wa vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia EPP hatua iliyomlazimisha Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk Donald Tusk, kufanya mazungumzo usiku kucha kutafuta makubaliano ya kumuunga mkono mgombea mmoja. Waandishi wa habari walisubiri usiku wote kupata habari katika ukumbi wa Baraza la Ulaya, huku wengine wakisinzia na kubwaga vichwa vyao kwenye meza.

Rais wa Bunge la Ulaya Antonio Tajani
Rais wa Bunge la Ulaya Antonio TajaniPicha: European Union/EP

Rais wa Bunge la Ulaya Antonio Tajani, ameitetea kanuni ya mgombea wa juu yaani Spitzenkandidat.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Brussels, Tajani alisema mfumo wa Spitzenkandidat yaani mfumo unaozingatia kiongozi wa muungano aliyepata kura nyingi ndio unaofaa, kwa maana kwamba mgombea anayeongoza anapaswa kutoka kwenye kambi ya kisiasa iliyopata kura nyingi zaidi kwenye chaguzi za Ulaya.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema mkutano bado unaendelea lakini wanaelekea kuridhia wagombea watatu kuchukua nafasi muhimu za usimamizi wa masuala ya mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya kwa miaka mitano ijayo.

Wagombea wanaotazamiwa kuchukua nafasi hizo za juu ni pamoja na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uholanzi wa Frans Timmermans ambaye anatazamiwa kuchukua wadhfa wa Rais wa Umoja wa Ulaya, Kristalina Georgieva wa Bulgaria huenda akamrithi Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk.

Wengine walio katika mstari wa mbele wa kupata nyadhfa hizo za juu ni  Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel na Kamishna wa Umoja wa Ulaya Margrethe Vestager kutoka Denmark ambaye anatazamiwa kuchukua nafasi ya mkuu wa sera za Mambo ya Nje wa umoja wa Ulaya.

Vyanzo:/RTRE/AP///p.dw.com/p/3LNIm