Ni Mwaka mmoja tangu mashambulio ya mabomu Kampala | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ni Mwaka mmoja tangu mashambulio ya mabomu Kampala

Watu 79 waliuawa katika mashambulio mawili katika eneo la mikahawa ya Waethiopia mjini humo.

Mnamo usiku wa tarehe 11 Julai 2010, washambuliaji waliokua wamejifunga mikanda iliojaa miripuko walijipenyeza katika umati wa watu waliokuwa wakiangalia fainali ya kandanda ya kombe la duniani na kujiripua. Lilikua shambulio baya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika Afrika mashariki katika kipindi cha miaka 12.

Kijana Ramadhani mwenye umri wa miaka 24 alinusurika katika hujuma hiyo iliofanywa katika makahawa wa Waethiopia, moja wapo ya maeneo mawili kulikotokea shambulio hilo, ambapo ndugu yake Ramadhani, Siraji aliuawa.

Akisimulia hali ilivyokuwa siku ile Ramadhani anasema, " Ndugu yangu alianguka kama mtu aliyelala usingizi, Mimi nilikua nimelala juu ya tumbo lake nikijaribu kumwamsha, na hadi leo najiuliza vipi yeye alifariki dunia na mimi ningali hai."

Ndugu hao wawili walikuwa wameipita mikahawa mingi tu na wakaamua kukaa katika mkahawa huo wa Waethiopia ambapo Siraji aliweza kujipenyeza na kupata mahala pa kukaa miongoni mwa viti vichache vilivyosalia. Ramadhani akakaa chini miguuni mwa nduguye.

Uganda imewakamata watu 36 wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulizi hayo ambapo waasi wa Somalia wa kundi la Al Shabab walidai kuhusika. Bado maafisa hawajaanza kusikiliza kikamilifu kesi za washukiwa ambao ni mwaka mmoja sasa wako korokoroni, wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi, mauaji na jaribio la kuuwa. Mara ya mwisho kufika mahakamani ilikuwa ni mwezi Novemba.

Wanaharakati wa haki za binaadamu na familia za watuhumiwa wameilaumu Uganda jinsi inavyoisimamia kesi hiyo, wakidai kuna hatua za kupelekwa watuhumiwa Uganda kinyume cha sheria, ukandamizaji, ucheleweshaji na pia siasa kuingizwa kati.

Lakini mwendesha mashtaka mkuu wa idara ya kimataifa ya uhalifu nchini Uganda Joan Kagezi anadai kwamba huenda kesi ikasikilizwa mwezi Agosti, akiongeza kwamba kwa viwango vya Uganda, kesi hiyo imekwenda haraka kwa sababu nyengine huchukua hadi miaka miwili au mitatu.

Miongoni mwa waliokamatwa ni mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini Kenya Al-Amin Kimathi ambaye alitiwa nguvuni Septemba mwaka jana alipowasili Kampala kusikiliza kesi za Wakenya wanaotuhumiwa kuhusika na mashambulizi hayo. Mashirika ya haki za binaadamu na chama cha wanasheria wa jumuiya ya madola Commonwealth, wametoa wito kutaka Kimathi aachiliwe huru kwa misingi ya kwamba kukamatwa kwake ni kinyume cha sheria, lakini Uganda imeukataa wito huo.

Nduguye Kimathi Onesmus Muriithi Imanene amesema kesi hiyo ina malengo ya kisiasa na kudai kwamba Uganda na Kenya zinashirikiana kuzuwia harakati za Kimathi.

Ingawa serikali ya Uganda inasema inaiachia sheria ifanye kazi, Imanene anasema anaamini bado ni kesi ya kisiasa, akigusia jinsi kaka yake alivyoendesha kampeni ya kupinga msimamo wa serikali ya Kenya kuikabidhi Uganda watuhumiwa 2007, kinyume cha sheria.

Wanamgambo wa Al-Shebab wanaosemekana kuwa na uhusiano wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, wamekula kiapo kufanya mashambulio zaidi ya mabomu mjini Kampala, wakizionya nchi jirani kutoiunga mkono serikali ya mpito ya Somalia. Uganda inakaribu nusu ya wanajeshi katika kikosi cha askari 9,000 wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, wakati nusu nyengine wanatoka Burundi. Al-Shebab wamedai kuwa mashambulio ya Kampala mwaka mmoja uliopita yalikua ni kulipiza kisasi kwa kuwepo wanajeshi hao nchini Somalia ambako waasi hao wanaendelea na mapigano kwa lengo la kuiangusha serikali ya mpito nchini humo.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman / AFP

Mhariri:Yusuf Saumu

 • Tarehe 12.07.2011
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/RZ50
 • Tarehe 12.07.2011
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/RZ50

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com