1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NASA yapeleka tena wanaanga mwezini baada ya miaka 50

Iddi Ssessanga APE, RTRE, AFPE
2 Aprili 2026

NASA yazindua misheni ya kihistoria ya Artemis II kuelekea mwezini, huku ESA ikilazimika kujadiliana upya nafasi yake baada ya Marekani kubadili mkakati wa anga.

https://p.dw.com/p/5BYUP
Marekani, Cape Canaveral 2026 | Uzinduzi wa misheni ya mwezi ya NASA, Artemis II
Wananchi walikusanyika mbali kidogo na kituo cha uzinduzi wa Misheni ya Artemis II ili kuwa sehemu ya hisotoriaPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Shirika la anga la Marekani, NASA, limezindua rasmi safari yake ya mwzini, kupitia chombo cha Artemis II, katika hatua muhimu ya safari za kumrejesha binadamu mwezini.

Uzinduzi huo umefanyika katika Kituo cha Safari za Anga cha Kennedy, ukibeba wanaanga wanne, ikiwa ni safari ya kihistoria ya kuuzunguka mwezi kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa.

Misheni hii ni sehemu ya mkakati mpana wa NASA wa kujenga uwepo wa kudumu wa binadamu mwezini, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kutua rasmi katika miaka ijayo.

Pamoja na mafanikio ya Artemis II, NASA imebadili mkakati wake kwa kusitisha mradi wa Gateway—kituo cha anga kilichopangwa kuzunguka mwezi.

Badala yake, sasa kipaumbele kinawekwa katika ujenzi wa makazi ya kudumu juu ya uso wa mwezi.

Marekani, Cape Canaveral 2026 | Misheni ya Artemis II | Wanaanga ndani ya kapsuli ya Orion kabla ya uzinduzi
Mwanaanga wa NASA Christina Koch akirekebisha kioo cha kofia yake ya anga akiwa karibu na mwanaanga wa Shirika la Anga la Canada (CSA) Jeremy Hansen ndani ya chombo cha Orion, kabla ya uzinduzi wa misheni ya Artemis II, Aprili 1, 2026.Picha: NASA TV/Handout/REUTERS

ESA yaanza mazungumzo mapya na NASA

Mabadiliko haya yamewaacha washirika wa kimataifa, hasa Shirika la Anga la Ulaya, ESA, wakiwa katika hali ya kutafuta mwelekeo mpya.

Mkurugenzi Mkuu wa ESA, Josef Aschbacher, amesema mazungumzo ya haraka yanahitajika ili kubaini nafasi ya Ulaya katika mpango mpya wa NASA.

Anatarajiwa kukutana na Jared Isaacman, mkurugenzi wa NASA, pamoja na timu yake kujadili ushiriki wa Ulaya katika misheni za kutua mwezini.

Mazungumzo hayo yataamua idadi ya nafasi za wanaanga wa Ulaya, masharti ya ushiriki na mchango wa teknolojia kutoka Ulaya.

Awali, ESA ilikuwa imehakikishiwa nafasi tatu katika misheni za Gateway.

Mpango huo ulihusisha mwanaanga wa Ujerumani, kisha wa Ufaransa na baadaye Italia.

Lakini kusitishwa kwa Gateway kunamaanisha nafasi hizo sasa zinahitaji kujadiliwa upya ndani ya mfumo mpya wa Artemis.

Marekani, Titusville 2026 | Watazamaji wakikusanyika kabla ya uzinduzi wa misheni ya Artemis II
Watu walikusanyika katika Space View Park kusubiri uzinduzi wa roketi ya kizazi kipya ya mwezini, Space Launch System (SLS), pamoja na kapsuli ya Orion, kama sehemu ya misheni ya Artemis II kutoka Kituo cha Anga cha Kennedy, Titusville, Florida, Marekani, Aprili 1, 2026.Picha: Marco Bello/REUTERS

Lengo: Mwanaanga wa Ulaya kutua mwezini

Licha ya changamoto, ESA imesisitiza kuwa inalenga kuona mwanaanga wa Ulaya akitembea juu ya uso wa mwezi.

Hata hivyo, mkakati wa muda mrefu ni kujenga uwezo wa kujitegemea katika safari za anga za binadamu.

Hii inahusisha uwekezaji katika teknolojia za anga, mifumo ya usafiri na miundombinu ya anga ya Ulaya.

Katika mbio hizi mpya za anga, mshirika mwingine wa NASA, shirika la safari za anga la Japan, JAXA, pia linatafuta nafasi yake.

Japan tayari ina mwanaanga aliyepangwa kushiriki katika misheni zijazo kabla ya baadhi ya Wazungu.

Hali hii inaonyesha wazi kuwa ushindani wa kimataifa katika safari za mwezi unaongezeka kwa kasi.

Marekani, Washington D.C. 2026 | Uzinduzi wa misheni ya Artemis II ukionyeshwa kwenye skrini ndani ya Ikulu ya White House
Uzinduzi wa misheni ya Artemis II ukionyeshwa kwenye skrini ndani ya Ikulu ya White HousePicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Enzi mpya ya safari za anga

Uzinduzi wa Artemis II umeashiria mwanzo wa enzi mpya ya safari za anga.

Lakini pia umefungua mjadala mkubwa kuhusu ushirikiano wa kimataifa, usawa wa fursa na mustakabali wa mataifa mbalimbali katika anga za mbali.

Kwa Ulaya, maamuzi yatakayofanyika sasa yataamua nafasi yake katika historia ya kurejea kwa binadamu mwezini.