1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshauri wa papa ahimiza kutazama upya suala la useja

6 Oktoba 2018

Mshauri wa juu wa Papa Francis ameonya Ijumaa kuwa Kanisa Katoliki liko hatarini kuingiliwa zaidi na polisi na serikali ikiwa halitashughulikia kashfa za unyanyasaji wa kingono kwa mapadri kwa kufanya mageuzi makubwa.

https://p.dw.com/p/365V1
Symbolbild Katholische Priester
Picha: picture-alliance/dpa/R. Haid

Kardinali Reinhard Marx ametoa wito wa kuwa na "mjadala wa wazi" ndani ya Kanisa Katoliki kuhusu ubasha, matumizi mabaya ya mamlaka na "useja na mafunzo ya upadri" kama sehemu ya muitikio kwa kadhia za ukiukaji wa kingono.

"Ikiwa hakuna hatua za kurekebisha zitakazochukuliwa na Kanisa -- na tunafanyia kazi hilo, tunapaswa kulifanyia kazi ---serikali haitakuwa na njia nyingine zaidi ya kuigilia," alisema Marx siku ya Ijumaa, akizungumzia uchunguzi unaoendelea dhidi ya viongozi wa Kanisaa katika mataifa kama Chile, Marekani na kwingineko.

Marx, mmoja kati ya washauri tisa wa kipadri wa papa Francis, alitoa matamshi yake katika uzinduzi wa shahada ya uzamili kuhusu ulinzi wa watoto katika chuo kikuu cha kichungaji cha Gregorian mjini Roma, ambako majesuti wanafundishwa. Uzinduzi wa kozi hiyo umekuja wakati Vatican imewakusanya mapadri zaidi ya 250 kujadili namna ya kuboresha uchungaji kwa vijana.

Kashfa duniani

Mkururo wa kashfa za ukiuaji wa kingono zinazolihusisha Kanisa Katoliki zimefichuliwa duniani katika miaka ya karibuni, ikiwemo nchini Ujerumani. Mwezi uliopita, ripoti iliyoagizwa na kanisa ilielezea kinagaubaga kwamba wachungaji wasiopungua 1,670 wa kikatoliki waliwanyanyasa kingono zaidi ya watoto 3,600 na vijana, wengi wao wa kiume, katika dayosisi za Ujerumani kati ya 1946 na 2014.

Deutschland Kardinal Marx
Kardinali Reinhard Marx, mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani anashauri suala la useja liangaliwe upya kutatua tatizo la unyanyasaji wa kingono ndani ya kanisa.Picha: Getty Images/AFP/D. Roland

"Maneno ya wasiwasi hayatoshi; lazima tuchukuwe hatua," alisema Marx kabla ya kuongeza kuwa visababishi vilikuwa vigumu zaidi kuliko kufanya kazi ya upadri bila kuoa. "Useja siyo chanzo cha ukiukaji; hali haiko hivyo hata kidogo."

Hata hivyo, Marx aliongeza kuwa kanisa, wakati likiandikisha, linapaswa kujiuliza iwapo udhaifu kama vile ubasha uliojificha, ukijumlishwa na useja, vinaweza kusababisha matatizo huko mbeleni.

Theluthi moja ndiyo waseja: Mtawa wa zamani

Anselm Bilgri, ambaye hadi mwaka 2004 alikuwa mtawa wa Kibenedict nchini Ujerumani, alisema katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Die Zeit kuwa "inakadiriwa kwamba theluthi moja ya mapadri wanavutiwa na mtu wa jinsia tofauti, na theluthi moja ndiyo wanajaribu kuheshimu kwa dhati (kwa kutekeleza sharti la useja).

Bilgri, mwandishi wa kitabu kilichochapishwa mwezi uliopita ambamo anatoa wito wa kukomesha useja kwa mapadri, alisema watu wengi hawana tena imani katika desturi hiyo, na hivyo kusababisha mapadri wengi kukidhi hamu zao za kingono kwa siri.

Utafiti wa mwaka 2015 uliofanywa na mwanathiolojia na mtaalamu wa magonjwa ya akili Eckhard Frick, uligundua kwamba miongoni mwa mapadri 4,200 na watumizi 8,600 wa kichungaji, ni moja tu kati ya wawili angeamua kuishi maisha ya useja ikiwa wangekua na fursa ya kuchagua tena.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape, dw

Mhariri: Yusra Buwayhid