1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa Covid-19: Vifo Ujerumani vyapindukia 100

23 Machi 2020

Ujerumani inatathmini hasara ya kiuchumi inayoweza kutokana na kusitishwa shughuli nyingi za kimaisha. Wakati huo huo, kuna uvumi unaozidi kuhusu mashimndano ya olimpiki ya 2020 yaliopangiwa kufanyika mjini Tokyo.

https://p.dw.com/p/3ZuYC
Deutschland Berlin Brandenburger Tor leer Ausgangsbeschränkung
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

- Ujerumani inaweza kupoteza karibu euro bilioni 500 ($538 bilioni) katika madhara ya mripuko wa virusi vya Corona na kufungwa kwa sehemu kwa shughuli za kimaisha.

- Msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amesema majibu ya vipimo vya virusi vya Corona yametoka na kuonyesha kuwa kiongozi huyo yuko salama. Steffen Seibert ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, "matokeo ya vipimo vya leo yameonyesha hana mambukizi" lakini vipimo zaidi vitafanyika katika siku zijazo."

Merkel alijiweka karantini nyumbani siku ya Jumapili jioni baada ya kufahamishwa kwamba daktari aliempatia chanjo alikutwa na virusi vya corona. Alipatiwa chanjo hiyo ya tahadhari dhidi ya homa ya mapafu siku ya Ijumaa.

- Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kuwekwa vituo vya afya vya dharura katika maeneo yalioathirika zaidi na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona - wa Covid-19.

- Idadi jumla ya vifo kutokana na janga la virusi vya corona - SARS-CoV-2 duniani vinakaribia 15,000, na watu wapatao 350,000 wameripotiwa kuambukizwa.

Merkel aendelea na shughuli zake nyumbani

Ni kweli Kansela Merkel yuko karantini, lakini hakuna kitu cha kuhofia. Kwa namna yoyote ile, si kwamba Ujerumani haina kiongozi, hata kama ikitokezea majibu ya vipimo yatakuja kuonesha kuwa ameambukizwa kirusi cha corona.

Katika hali ya kawaida, anaweza kuendelea na kazi zake za kiserikali akijihisi kwamba ana afya nzuri ya kufanya hivyo. Lakini endapo akiumwa kweli, baraza lake la mawaziri bado linaweza kuongoza nchi, maana mambo kama hutokezea na utaratibu wa kuyashughulikia upo.

Kifungu Nambari 69 cha Katiba ya Ujerumani kina kipengele kinachomtaka kansela kumteuwa waziri mmoja kuwa naibu wake. Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Waziri wa Fedha Olaf Schulz kutoka chama cha Social Democratic, ambaye mara kadhaa amewahi kumuwakilisha Kansela Merkel anapokuwa hayupo kwenye kazi zake, hata kama ni mzima. Matukio ya kawaida ni pale anapokuwa likizo ama ziara za nje kikazi. Katika hali kama hiyo, mathalani, naibu kansela huendesha vikao cha baraza la mawaziri ambavyo kawaida hufanyika kila Jumatano.

Berlin Bundeskabinett tagt ohne Merkel
Makamu wa Kansela ambaye pia ni waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz kutoka chama cha SPD akiwa ameketi karibu na kiti kitupu cha Kansela Merkel wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri, Jumatatu 23, 03.2020.Picha: picture-alliance/dpa/F. Bensch

Naibu Kansela ni jina lisilo rasmi na ambalo halimo kwenye katiba ya nchi. Lakini kwenye matumizi ya kawaida, neno hili limekuwa la kawaida, likimaanisha mbadala. Katika hali ya sasa, Kansela Merkel anaweza kinadharia kumteuwa mtu kutoka chama chake cha Christian Democratic Union, CDU au kinachoshirikiana nacho cha Christian Social Union, CSU kutoka jimboni Bavaria. Lakini kimatendo, naibu kansela huwa kawaida anatokea chama cha pili kwenye serikali ya mseto, na kwa sasa chama hicho ni cha Social Democtaic, SPD, chake Olaf Scholz.

Ibara ya 8 ya muongozo wa uendeshaji wa serikali kuu ya shirikisho inasema kwamba waziri huyo wa fedha anaweza kumuwakilisha Merkel, ambaye kwa sasa yuko kwenye karantini nyumbani kwake, kwa kipindi kirefu zaidi kadiri inavyohitajika. Na kama "kwa ujumla atakuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake", Scholz anaweza kumwakilisha bosi wake "kwenye kipindi chote", hadi hapo mwenyewe Merkel "atakapoamuwa ukomo wa kuwakilishwa."

Berlin Bundeskabinett tagt ohne Merkel
Wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Ujerumani wakikutana katika ofisi ya Kansela kwa ajili ya kikao cha Baraza bila kuwepo Kansela Angela Merkel, Machi 23.2020.Picha: picture-alliance/dpa/F. Bensch

Mawaziri wengine wote wa serikali wana manaibu wao pia. Kuna kifungu pia kimeundwa pale ambapo kwenye mgogoro kama huu wa corona, ambapo kansela na naibu wake kwa wakati mmoja wamejikuta wakishindwa kutimiza majukumu yao. Mwakilishi anatajwa kwa kila mjumbe wa baraza la mawaziri ndani ya muongozo wa uendeshaji serikali. Majukumu ya Olaf Schulz yatachukuliwa na Waziri wa Uchumi Peter Altmaier kutoka chama cha CDU, chake Kansela Merkel.

Hata hivyo, haijawahi kutokea nchini Ujerumani kwa kansela kutokuwapo muda mrefu kiasi hicho cha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kiserikali.

Mwandishi: Marcel Fürsteneau