1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kimataifa juu ya ukimwi na juhudi zaidi dhidi ya ugonjwa huo

Nijimbere, Gregoire5 Agosti 2008

Mahitajio ya fedha za kugharimu mipango ya kupambana na ugonjwa hatari wa ukimwi na maradhi yanayokwenda sambamba na ukimwi yaliongezeka sana mwaka jana na kufikia bilioni 6,4 za dola za kimarekani.

https://p.dw.com/p/Eqmq
Wajumbe mkutanoni mjini MexicoPicha: picture-alliance/ dpa

Maombi ya gharama za kupambana na maradhi ya ukimwi na maradhi yanayokwenda sambamba mara nyingi na ukimwi ikiwa ni pamoja na kifua kikuu na malaria, yaliongezeka mara tatu mwaka jana kulinganisha na miaka michache iliyopita. Fuko la dunia la kupambana na maradhi ya ukimwi limesema lilipokea maombi kutoka nchi 97 kutoka pembe nne za dunia yanayofikia bilioni 6,4 za dola za kimarekani. Maombi hayo yalikuwa juu ya kueneza mipango ya kinga dhidi ya ukimwi, vyandarua kupambana na malaria na kueneza madawa dhidi ya kifua kikuu katika hospitali na zahanati.Fuko hilo la dunia la kugharimu mipango ya kupambana na ukimwi, limeshatoa bilioni 11,4 za dola za kimarekani kwa nchi 136 tangu liundwe mwaka 2002. Na hiyo ni sawa na robo ya misaada yote ya kimataifa katika kupambana na ukimwi, theluthi mbili kuhusu kifua kikuu na robo tatu kuhusu malaria.

Maelezo hayo yaliyotolewa katika mkutano wa kimataifa juu ya maradhi ya ukimwi unaoendelea mjini Mexico, yanaonyesha kwamba juhudi za kupambana na ukimwi zinagharimu fedha nyingi.

Licha ya gharama hizo kubwa zinazohitajika katika kukabiliana na maradhi ya ukimwi, wajumbe mkutanoni walisema hawana budi kuendelea na vita dhidi ya ukimwi kwani kamwe maradhi hayo yasipuuzwi kama alivyoshauri mkurugenzi wa kitengo cha Umoja wa mataifa cha kupambana na ukimwi Peter PIOT.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton ni miongoni mwa wajumbe waliotoa hutuba zao. Katika hutuba yake ambayo ilikaribishwa sana, Bill Clinton amesema maradhi ya ukimwi ni dragoni mkubwa kuwahi kutokea na ambae atauliwa na ma milioni ya wanajeshi wa nchi kavu akimanisha ushirikiano wa watu wote duniani katika kupambana na ukimwi. Bill Clinton ambae aliwasili katika mkutano wa mjini Mexico akitokea ziarani katika nchi nne za bara la Afrika zinazokabiliwa zaidi na maradhi ya ukimwi, alisema bado kuna mengi ya kufanya katika kuimarisha kinga, kueneza madawa ya kudhohofisha virusi vya ukimwi na kuimarisha sekta ya afya kwa jumla. Kuna watu milioni 1,4 wanaoishi na virusi vya ukimwi wanaonufaika na madawa yanayogharimiwa na Shirika la Bill Clinton.

Kwa upande wake,tajiri mashuhuri kutoka Mexico, Carlos Slim ambae inakisiwa ni tajiri wa pili duniani, alitoa milioni 50 za dola za kimarekani kwa ajili ya miradi ya kupambana na ukimwi nchini Mexico, Colombia na Peru.

Kulingana na Shirika la Umoja wa mataifa la kupambana na ukimwi, takriban bilioni 10 za dola za kimarekani zilitumiwa mwaka jana katika juhudi za kupambana na ukimwi duniani lakini bado kunahitajika bilioni 8 zaidi kila mwaka kukidhi mahitajio yote katika sekta hiyo.