1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya maendeleo na uongozi mzuri

23 Septemba 2009

Rais wa Marekani Barack Obama alipotembelea rasmi nchi za Kiafrika mapema mwaka huu alisema, ufisadi na serikali za mabavu ni uovu unaohatarisha maendeleo katika bara zima la Afrika.

https://p.dw.com/p/JnY3
President Barack Obama delivers speech at Nellis Air Force Base in Las Vegas, Wednesday, May 27, 2009. (AP Photo/Isaac Brekken)
Rais wa Marekani,Barack Obama.Picha: AP

Kwa maoni yake suluhu ni serikali iliyo na uongozi bora. Kwa hivyo, katika siku zijazo Marekani itatoa msaada wa maendeleo kwa serikali zinazowajibika na itazitenga zisizofanya hivyo. Je, uongozi bora ndio suluhisho?

Misaada ya maendeleo mara nyingi, hushindwa kufanikiwa kwa sababu mbali mbali. Sababu moja kuu ni uongozi mbaya- kwa maneno mengine sababu ni ufisadi,matumizi mabaya ya mamlaka,ukiukaji wa haki za binadamu na kutokuwepo hali ya uwazi. Hiyo ni mifano michache tu.

Lengo kuu la misaada ya maendeleo ni wafadhiliwa hatimae kuweza kujitegemea. Lengo hilo linaweza kufikiwa ikiwa mazingira ya kisiasa ni barabara. Lakini ikiwa madikteta, kwanza kabisa wanafikiria kujaza mifuko yao na kupeleka pesa katika akaunti za siri nchini Uswissi na hupendelea kuongeza bajeti ya jeshi ili kujiimarisha madarakani na kuwalenga wakosoaji wake, basi ni kosa kuwekeza katika nchi kama hiyo, hata kwa mtazamo wa kiuchumi.

Katika enzi ya vita baridi na mivutano kati ya kambi ya magharibi na ya mashariki, hata serikali za kidikteta zilipewa misaada ya maendeleo - kilichokuwa muhimu ni kwamba serikali hiyo ilielemea kambi fulani. Orodha ya madikteta waliopokea misaada ni ndefu - kuanzia Idi Amin wa Uganda hadi Ferdinand Marcos wa Ufilipino na Anastasio Somoza nchini Nicaragua. Pesa zilimiminwa kwa mabilioni katika nchi zilizotawaliwa na madikteta, bila ya kuona matokeo ya maana. Mbaya zaidi ni kwamba misaada hiyo ya pesa haikutumiwa tu na madikteta hao waovu, kujijengea makasri ya fahari, bali ilitumiwa kujiimarisha kisiasa ili kubakia madarakani. Pasingekuwepo misaada hiyo ya maendeleo, ulimwengu ungeepukana na baadhi ya madikteta.

Kwa hivyo, misaada ya maendeleo lazima ifungamanishwe na masharti ya kisiaasa ama sivyo, misaada hiyo haitokuwa na maana. Kwa ufupi, sharti ni uongozi bora:- yaani serikali iliyo na uongozi mzuri.demokrasia,hali ya uwazi na inayojumuisha jamii. Lakini wakosoaji wanasema, huo ni mfumo mpya wa ukoloni. Wanauliza kwa nini nchi za barani Afrika,Asia na Latin Amerika zifuate mfumo wa maadili wa nchi za magharibi? Kinyume ndio sahihi: kwani maadili kama haki za binadamu, uhuru wa kueleza maoni, na utawala wa kisheria , si haki ya mataifa tajiri bali ni lazima kuwa halali kote duniani. Itakuwa ujinga kuamini kuwa misaada ya maendeleo itatosha kueneza mfumo huo wa maadili kote ulimwenguni. Lakini misaada inaweza kuwa sehemu muhimu ya mfumo huo.

Takriban miaka kumi iliyopita,katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan alisema, labda uongozi bora ndio kilicho muhimu kabisa katika jitahada za kuondosha umasikini na kuleta maendeleo. Hapo wala hakuna cha kuongezea kwani aliyotamka ni sahihi kabisa.

Mwandishi: S.Golte/ZPR/P.Martin

Mhariri: M. Abdul-Rahman