Merkel mgombea rasmi wa CDU na CSU | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel mgombea rasmi wa CDU na CSU

Viongozi wa chama cha kihafidhina cha kansela wa Ujerumani Angela Merkel wameweka kando tofauti zao na kuunga mkono juhudi  zake za kuwania muhula wa nne madarakani katika uchaguzi mkuu mwezi Septemba.

Angela Merkel und Horst Seehofer (Getty Images/J. Simon)

Angela Merkel (kushoto) na kiongozi wa CSU Horst Seehofer

Chama  cha  kansela  Angela  Merkel  cha  Christian Democrats CDU  na  washirika  wake  wa  jimbo  la  Bavaria  chama  cha Christian Social Union CSU, vimeamua  katika  mkutano  wao  wa pamoja  mjini  Munich  kumuunga  mkono  haraka  akiwa  kama mgombea  wao  kwa  tikiti  ya  vyama  hivyo  katika  uchaguzi  wa mwezi  Septemba  ili  kusaidia  kuzuwia  ongezeko  la  uungwaji mkono  kwa  chama  cha  Social  Democratic  SPD.

Deutschland PK Martin Schulz SPD Kanzlerkandidat (picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka)

Mgombea wa chama cha SPD Martin Seehofer

Ongezeko  la  haraka  la  uungwaji  mkono  kwa  chama  cha upinzani  cha  SPD linakuja  baada  ya  chama  hicho cha  siasa  za wastani  za  mrengo  wa  kushoto  kuishangaza  medani  ya  kisiasa katika  taifa  hilo  kwa  kumteua  spika  wa  zamani  wa  bunge  la Ulaya  Martin Schulz  kuongoza  kampeni  zake  za  uchaguzi.

Wakati  Schulz ni  mtu  maarufu  katika  medani  ya  siasa  barani Ulaya, hafahamiki  sana  ndani  ya  Ujerumani,  na  kusababisha wadadisi  wa  masuala  ya  siasa   kudokeza  kwamba  nafasi  yake kama  mtu  asiyefahamika  imeongeza  mvuto  wake.

Chama  cha  kansela  Merkel  cha  CDU  kilimuunga  mkono  kama mgombea  wake  wa  ukansela  katika  mkutano  wa  chama  hicho Desemba  mwaka  jana, lakini  chama  cha  CSU  kilikuwa hakijatangaza  rasmi  uungaji  wake  mkono  hadi  katika  mkutano huo  leo  mjini  Munich.

"Tunatofautiana  katika  suala  la  ukomo wa wahamiaji. Tumeeleza kuhusiana  na upinzani  huu kwamba  tunaheshimu  upinzani, lakini pia  hatujazuwia upinzani. Nafikiri  hili  pia  ni  sahihi na halitafanikiwa."

Deutschland Martin Schulz und Angela Merkel (picture alliance/dpa/U. Baumgarten)

wagombea wa chama cha CDU na SPD

Washirika wamaliza tofauti  zao

Mahusiano  baina  ya  washirika   hao  wawili  hayajakuwa  ya utulivu. Kiongozi  wa  chama  cha  CSU  na  waziri  mkuu  wa  jimbo la  Bavaria  Horst Seehofer  aliongoza  wimbi  la  ukosoaji  kuhusiana na  jinsi  Merkel  alivyoshughulikia  mzozo  wa  wakimbizi  baada  ya kufungua mipaka ya  Ujerumani  mwezi  Septemba  2015 kuwaruhusu  mamia  kwa  maelfu  ya  wakimbizi  na  waombaji hifadhi  pamoja  na  wahamiaji  kuingia  katika  taifa  hilo. Lakini  leo alisema.

Deutschland Spitzentreffen in München: Koalition berät Sicherheitspaket (reuters/M. Dalder)

Kansela Angela Merkel

"Kulikuwa  na  tofauti lakini wakati  wote  tuliheshimiana  na  bila kudharauliana. Na leo imekuwa  wazi . Tunaingia  katika  uchaguzi pamoja."

Tangu  wakati  huo, Merkel  mwenye  umri  wa  miaka  62, amerudia mara  kwa  mara  kupuuzia  madai  ya  Seehofer  kwamba  aweke ukomo  kwa  idadi  ya  wakimbizi  wanaoingia, na  hali  hiyo ikasababisha  mgawanyiko  baina  ya  CDU na CSU.

Wachunguzi  wa  maoni  ya  wapiga  kura  wamesema  hali  ya  wasi wasi   kati ya  CDU  na  CSU  kuhusiana  na  msimamo wa  Merkel kwa  wakimbizi umechangia  kuporomoka kwa  kiwango  cha  juu kwa  uungwaji  mkono  wa  vyama  vyote  hivyo. Suala  la  uhamiaji linaonekana  litaendelea  kuleta  mgawanyiko  ambapo CDU na CSU pia  vitapata  changamoto  kubwa  kutokana  na  kupanda  kwa chama  cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia, cha Alternative for Germany AfD.

Deutschland Banz Horst Seehofer (picture-alliance/dpa/N. Armer)

Kiongozi wa chama cha CSU Horst Seehofer

Mchakato  wa  kuelekea  uchaguzi  wa  mwezi  Septemba utaongozana  na  chaguzi  kadhaa  za  majimbo, ikiwa  ni  pamoja  na jimbo  kubwa  kabisa  nchini  Ujerumani  la  Nort-Rhine Westfalia mwezi  Mei. Chaguzi  kadhaa  zimeonesha  ongezeko  la  uungwaji mkono  kwa  Schulz  mwenye  umri  wa  miaka 61 tangu  alipoteuliwa kuwa  mgombea  wa  chama  cha  SPD  katika  wadhifa  wa ukansela, Jumanne  iliyopita  pamoja  na  chama  chenyewe.

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / dpae

Mhariri: Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com