Merkel awataka Wajerumani washikamane | Masuala ya Jamii | DW | 31.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Merkel awataka Wajerumani washikamane

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anauita mmiminiko wa wakimbizi na utangamano wao kama "fursa ya baadaye" akiwataka Wajerumani kujifunza kutokana na makosa ya zamani wakati huu wa mzozo wa wakimbizi.

Kansela Angela Merkel akihutubia taifa kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha 2016.

Kansela Angela Merkel akihutubia taifa kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha 2016.

Akitupia jicho lake kwenye mzozo wa wakimbizi, Kansela Merkel anasema kwamba kama kuna kitu kimoja muhimu kabisa kuliko yote kwa mwaka 2016 nchini Ujerumani, basi kitu hicho ni "mshikamano wetu."

"Ni muhimu kwamba hatuachi tugawiwe. Sio kwa vizazi, sio kwa makundi ya kijamii, na sio kwa wale waliokuwapo hapa kabla na wale walio raia wapya," anasema Kansela Merkel kwenye hotuba hiyo inayoandaliwa maalum mwishoni mwa kila mwaka kuuaga mkongwe na kuukaribisha mpya.

Watu hawapaswi kuwafuata "wale wenye mioyo migumu, au hata chuki kwenye nafsi zao, na wanaojipa haki ya kuitwa Wajerumani peke yao na kuwatenga wengine," alihoji Merkel bila ya kulitaja kwa jina kundi la PEGIDA, ambalo kirefu chake ni "Wazalendo wa Ulaya Dhidi ya Kusambaa Uislamu."

Tujifunze kwa makosa ya zamani

Kansela Angela Merkel akipiga picha na wakimbizi wa Syria wanaoingia Ujerumani.

Kansela Angela Merkel akipiga picha na wakimbizi wa Syria wanaoingia Ujerumani.

Badala yake, alisema Wajerumani wanapaswa kujiamini na kuwa huru, wenye kuwazingatia na kutangamana na wengine, kwani ili utangamano wa kijamii ufanikiwe "tunapaswa kujifunza kutokana na makosa ya zamani. Mila zetu, desturi zetu, hamu yetu ya kusimamisha haki, lugha yetu, sheria zetu, kanuni zetu," alisema zinawahusu wote wanaotaka kuishi Ujerumani.

Kansela huyo alitilia mkazo kwamba kila nchi ambayo imefanikiwa kwenye kujenga utangamano na wahamiaji wapya imefaidika na jambo hilo kiuchumi na kijamii. Na kwa hilo, akaweka wazi kwamba anategemea wakimbizi wengi zaidi watabakia Ujerumani na sio kurejea makwao.

Wakati huo huo, alisema Ujerumani inalifanyia kazi suala la kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nje ya Ulaya, kuugeuza uhamiaji haramu kuwa uhamiaji halali, na kuendeleza mapambano dhidi ya vyanzo vikuu vya mzozo wa wakimbizi ili kufikia lengo la muda mrefu la kupunguza idadi ya wakimbizi wapya katika siku zijazo.

Sehemu kubwa ya hotuba hiyo imejikita kwenye mzozo wa wakimbizi, ambapo Kansela Merkel anawashukuru watu waliojitolea kuwasaidia wakimbizi "kwa moyo wao usio na kifani na usiomithilika." Hata hivyo, anasema ni jambo lililo wazi kwamba mmiminiko wa watu wengi kama hawa "utahitaji mengi kutoka kwetu, kwa maana ya muda, nishati na fedha."

Tusemeni pamoja: 'Tunaweza kufanya hivyo'

Maandamano ya kundi la PEGIDA dhidi ya wakimbizi na wageni kutoka mataifa ya Kiislamu nchini Ujerumani.

Maandamano ya kundi la PEGIDA dhidi ya wakimbizi na wageni kutoka mataifa ya Kiislamu nchini Ujerumani.

Mwishoni mwa hotuba yake, Kansela Merkel anarejea kaulimbiu yake: Tunaweza kufanya hivyo, kwa sababu Ujerumani ni taifa imara. Sambamba na wafanyakazi wa misaada kwa wakimbizi, kansela huyo pia anasema anawashukuru wanaume na wanawake wanaohudumu kwenye vikosi vya jeshi la Ujerumani "kutoka kwenye chembe cha moyo" wake kwa "kuiweka miili na maisha yao hatarini kwa ajili ya kupigania imani yetu, usalama wetu na uhuru wetu," katika vita dhidi ya magaidi waliojitangazia wenyewe "Dola la Kiislamu."

Hata hivyo, changamoto alizozitaja kwenye hotuba yake ya kuukaribisha mwaka 2015, kama vile mapinduzi ya kidijitali na ulinzi wa mazingira, hazikutajwa mwaka huu, kama ilivyokuwa pia kwa mzozo wa sarafu ya euro.

Badala yake, nafasi yake ikachukuliwa na ushabiki wake mkubwa kwa timu ya taifa ya mpira wa miguu, akiitakia kheri kwenye Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya litalochezwa nchini Ufaransa mwaka 2016, ambako "mabingwa wetu wa dunia wanataka pia kuwa mabingwa wa Ulaya."

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW English
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com