Mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati yaendelea
15 Septemba 2010Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais Mahamoud Abbas wa Palestiana leo yameingia katika siku ya pili, mjini Jerusalem. Mazungumzo hayo ambayo ni duru ya pili yalianza jana huko Sharm el-Sheikh-Misri. Lakini ujenzi wa vitongoji vya makaazi ya Wayahudi , ambao unatishia kuivunja duru ya hivi sasa ya mazungumzo ya kutafuta amani ya mashariki ya kati yanayosimamiwa na Marekani , umewakasirisha Wapalestina pamoja na mataifa mengi ya Kiarabu tangu pale ujenzi huo ulipoanza miaka 40 iliyopita.
Wapalestina wanaona kuwepo kwa Waisrael nusu milioni katika vitongoji zaidi ya 120 vilivyotawanyika katika maeneo yanayokaliwa kimabavu na Israel pamoja na eneo lililotekwa la Jerusalem ya mashariki ni tishio kubwa dhidi ya kuundwa kwa taifa la baadae la Wapalestina.
Jumuiya ya kimataifa , ikiwa ni pamoja na mshirika wa karibu wa Israel , Marekani inatambua kuwa ni kinyume na sheria ujenzi wa makaazi hayo, lakini makaazi hayo yameendelea kuongezeka na kupanuka katika wakati wa kila serikali ya Israel tangu kuanza kwa uvamizi huo Juni 1967.
Katika muda wa miezi michache baada ya Israel kuyakamata maeneo kadha ya Waarabu katika vita vya siku sita vya ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza pamoja na Jerusalem ya mashariki, ardhi ambayo hivi sasa inatarajiwa kuundwa taifa la Wapalestina , kazi ilianza katika ujenzi wa makaazi ya kwanza ya Gush Etzion, karibu na Jerusalem.
Viongozi wa harakati za walowezi wa Kiyahudi wanaliona eneo la ukingo wa magharibi na Jerusalem ya mashariki kuwa ni sehemu ya taifa la Israel , ambayo wamepewa Wayahudi na Mungu, na wanaviona vitongoji hivyo vya walowezi kuwa ni hali halisi katika maeneo hayo kuweza kuzuwia kuondolewa.
Tangu pale zilipofanyika hatua za kuleta amani za mjini Oslo mwaka 1993, idadi ya walowezi imeongezeka kwa karibu mara tatu kwa kuhamasishwa na viongozi wa Kiyahudi wenye msimamo , ikiwa ni pamoja na waziri mkuu Benjamin Netanyahu na waziri mkuu wa zamani Ariel Sharon , ambaye ni maarufu kama, "baba wa harakati za walowezi". Akizungumzia mkutano uliofanyika huko Sharm el Sheikh nchini Misri, rais wa Israel Shimon Perez alionyesha matumaini kuhusu mikutano hiyo.
Kikao cha jana mjini Sharm el Sheikh kilikuwa bora zaidi kuliko watu wote waliokuwa na shaka na wasio na matumaini walivyotarajia. Siamini kuwa unaweza kutatua matatizo haya kwa mikutano miwili au mitatu, lakini ulikuwa mwanzo mzuri na kuna hali ya kuendelea. Na hisia zangu nilipozungumza na waziri mkuu wetu mkuu pamoja na viongozi wengine , ni kwamba kuna hisia kuwa tufanye kile kinachowezekana kwa ajili ya hali bora ya pande zote zinazohusika.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amewaunga mkono viongozi wa Israel na Palestina leo kabla ya mazungumzo yao yanayojaribu kuvunja mkwamo kuhusiana na ujenzi wa vitongoji hivyo vya walowezi katika maeneo yanayokaliwa kwa nguvu na Israel ya ukingo wa magharibi.
Huu ndio wakati, na hawa ndio viongozi, amesema Clinton kabla ya kuonana na waziri mkuu Benjamin Netanyahu na rais Mahmoud Abbas, ambao wameanza tena mazungumzo yao ya moja kwa moja ya kutafuta amani wiki mbili zilizopita baada ya kutokufanyika kwa muda wa miezi 20.
Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE / AFPE
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman