Mashambulio ya kigaidi mjini Jakarta, Indonesia yamefanywa na watu wawili waliojitoa mhanga. | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashambulio ya kigaidi mjini Jakarta, Indonesia yamefanywa na watu wawili waliojitoa mhanga.

Polisi yagundua kuwa mabomu hayo yalitengenezwa katika chumba kimoja kwenye hoteli ya Marriott.

default

Ndugu wa watu waliokufa katika mashambulio ya mabomu ya Bali, Indonesia mwaka 2005.


Polisi nchini Indonesia wamesema kuwa mashambulio ya mabomu yaliyotokea leo asubuhi katika hoteli mbili za kifahari mjini Jakarta, yamefanywa na watu wawili waliojitoa mhanga. Mkuu wa polisi wa nchi hiyo, Bambang Hendarso Danuri, amesema uchunguzi wa polisi umegundua kuwa mabomu hayo yalitengenezwa katika moja ya hoteli iliyoshambuliwa ya Marriott.

Kwa mujibu wa Danuri, bomu hilo lilitengenezwa katika Hoteli ya JW Marriott chumba namba 1808, chumba ambacho kilikuwa sehemu kuu ya upangaji wa mashambulio hayo, yaliyosababisha vifo vya watu tisa na wengine zaidi ya 50, wakiwemo raia wa kigeni kujeruhiwa. Amesema mabomu yaliyoshambulia hoteli ya Marriott, na ile ya jirani ya Ritz-Carlton yanafanana na kwamba yalisafirishwa kutoka chumba hicho cha hoteli ya Marriott.

Maiti sita zimekutwa katika hoteli ya Marriott, maiti mbili katika hoteli ya Ritz-Carlton na maiti ya tisa iliongezeka baada ya majeruhi mmoja kufia hospitalini. Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, rais wa kampuni ya saruji ya Uswisi iliyopo nchini Indonesia, Timothy Mackay, raia wa New Zealand, ni miongoni mwa waliouawa. Pia inasadikiwa kuwa raia watatu wa Australia ni miongoni mwa watu waliokufa.

Aidha, Danuri amesema bomu moja ambalo lilikuwa halijaripuka limekutwa katika chumba hicho, ambalo baadaye liliteguliwa na polisi. Hata hivyo, amesema bado ni mapema mno kueleza nani anahusika na mashambulio hayo ya kigaidi, ingawa idara ya polisi inayokabiliana na ugaidi, imeeleza kuwa huenda kundi la kigaidi la Jemaah Islamiyah likawa ndilo linahusika na mashambulio hayo.

Rais wa Indonesia, Susilo Bambang Yudhoyono, amelaani vikali mashambulio hayo na kusema kuwa nchi yake haitawaachia watu wanaofanya uhalifu pamoja na mauaji kukimbia.

Akizungumza na waandishi habari, Rais Yudhoyono amesema kuwa watu hao waliofanya mashambulio hayo hawana utu na hawajali kuhusu uharibifu wa mali za nchi hiyo kutokana na vitendo vyao hivyo vya kigaidi, ambavyo kwa kiasi kadhaa vitaathiri uchumi wa nchi hiyo, biashara, utalii na taswira ya Indonesia katika ulimwengu.

Nchi mbalimbali zimekuwa zikilaani vikali mashambulio hayo ya mjini Jakarta, ambapo hadi sasa zimeahidi kutoa ushirikiano kwa Indonesia. Nchi hizo ni pamoja na Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Australia. Mbali na nchi hizo, pia Umoja wa Ulaya na Jumuia ya nchi za Kiislamu (OIC), zimelaani mashambulio hayo ya kigaidi.

Katika hatua nyingine, kutokana na mashambulio hayo ya kigaidi mabingwa wa ligi ya Uingereza (Premier League), Manchester United imeahirisha mchezo wake wa kirafiki na timu ya Indonesia ya All Star, mchezo uliopangwa kufanyika Jumatatu ijayo. Wachezaji wa timu ya Manchester United walikuwa wafikie katika hoteli ya Ritz-Carlton.

Indonesia imekuwa ikigubikwa na mfululizo wa mashambulio ya kigaidi likiwemo lile la mwaka 2002 na 2005 katika kisiwa cha Bali na kusababisha vifo vya watu 200. Lakini kwa takribani miaka mitatu nchi hiyo haijakumbwa na shambulio lolote la kigaidi. Pia, hii ni mara ya pili kwa hoteli ya Marriott kushambuliwa ambapo Agosti 5, mwaka 2003 yalifanyika mashambulio mengine na kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 150, kujeruhiwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE/)

Mhariri: Othman Miraji • Tarehe 17.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Irkl
 • Tarehe 17.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Irkl
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com