1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G-7 Elmau

1 Juni 2015

Urusi kuwapiga marufuku baadhi ya wanasiasa wa Umoja wa Ulaya kuitembelea nchi hiyo,hatua za usalama kuelekea mkutano wa viongozi wa G-7 Elmau na malalamiko kwa kuchaguliwa upya Joseph Blatter kuiongoza FIFA magazetini

https://p.dw.com/p/1Fa22
Picha ya kasri la Elmau ,utakakofanyika mkutano wa viongozi wa mataifa Saba tajiri kiviwanda mwaka huu wa 2015

Tuanzie lakini Moscow ambako uamuzi wa viongozi wa ikulu ya Urusi-Kremlin, kutangaza orodha yenye majina ya wanasiasa wa Umoja wa ulaya wanaozuwiliwa kuingia nchini humo, unakosolewa na kuangaliwa wakati huo huo kama jibu la vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa nchi hiyo.Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linaandika:"Vikwazo upande huu na upande ule marufuku ya kusafiri na kujadiliana.Mtindo wa enzi za kale unarejea upya.Lakini Umoja wa Ulaya pia ni wa kulaumiwa.Watu wanaonyesha kusahau kwamba wabunge wa Urusi wamepigwa marufuku tangu zamani ya kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya na akonti zao kufungwa.Malalamiko hayakuwa makubwa.Na hivi sasa hali iwe hivyo hivyo .Orodha ya Kremlin isikuzwe,seuze tena marufuku ya kusafiri kutoka pande zote mbili hayendi mbali sana.Na pengine kutangazwa orodha hiyo kumetokea wakati muwafak kwa pande zote mbili kustaghafiru,kutambua kuwa ni makosa kumfukuza mtu na kwa namna hiyo kuzitumbukiza orodha hizo kabatini."

Hatua kali za usalama kwaajili ya G7

Hatua za usalama zinazochukuliwa kuelekea mkutano wa viongozi wa mataifa saba tajiri kiviwanda G-7 zinawazungusha kichwa wakaazi wa kijiji cha kusini mwa Ujerumani Elmau.Gazeti la "Münchner Merkur" linaandika:"Inawezekana kwamba picha za mandhari ya kuvutia ya Elmau zikawapatia tija wenye kumiliki hoteli.Mradi si raia wa kawaida katika jimbo la kusini la Bavaria.Anakereka na hafurahikii hata kidogo gharama kubwa kubwa zote hizi.Sawa mkutano wa kilele wa G-7 unastahiki kuitishwa-hilo hakuna anaebisha.Mazungumzo ya ana kwa ana ya viongozi hayana mbadala.Lakini mahala pa kuitisha mazungumzo hayo,wamekosea- sio huku.Kilichosaalia kwasasa ni kuvumilia."

Joseph Blatter anasema hatosahau

Mada ya mwisho magazetini inahusiana na malalamiko baada ya Sepp Blatter kuchaguliwa kuliongoza kwa mara nyengine tena shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA,licha ya shirikisho hilo kugubikwa na tuhuma za rushwa.Gazeti la Donaukurier linaandika:"Badala ya kushukuru kwa kuondoka bila ya madhara makubwa angalao kwa sasa katika kinyang'anyiro cha kupimana nguvu dhidi ya shirikisho la kabumbu barani Ulaya UEFA,mwenyekiti wa FIFA anatoa maneno makali:Nnawasamehe wote,lakini sisahau"-ndio kauli aipendayo hivi sasa.Ukimchunguza kwa makini raia huyo wa Uswisi hutokosa kutambua:hapa anazungumzia kuhusu maisha yake,kuhusu kile alichokifanya maishani mwake.Hakuna,isiüpokuwa muimla tu ndie anaezungumza kama yeye."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman