Marekani yapania kuwaandama magaidi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Marekani yapania kuwaandama magaidi

Rais Barack Obama anasema watawasaka magaidi wa Al Qaida kokote kule waliko

Gaidi mtuhumiwa Umar Farouk Abdulmutallab

Gaidi mtuhumiwa Umar Farouk Abdulmutallab

Njama iliyoshindwa ya kuiripua ndege ya shirika la ndege la Delta la Marekani imesababisha macho ya walimwengu kuelekezwa Yemen ambako mtandao wa kigaidi wa Al Qaida unazidi kupata nguvu.

Gaidi mtuhumiwa Umar Farouk Abdulmuttalab alikua pia Yemen mara mbili mwaka huu, kwanza mwezi wa Agosti na baadae mapema mwezi huu kabla ya kufanya njama hiyo ya kutaka kuiripua ndege ya shirika la ndege la Marekani Delta. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Yemen amesema mjini Sanaa kijana huyo alipata viza ya kusomea lugha ya kiarabu katika taasisi moja ya mjini Sanaa.

Umar Farouk Abdulmuttalab amelihakikishia shirika la FBI amejiunga na kambi za mazoezi za mtandao wa Oussama Ben Laden nchini Yemen.

Hata familia yake imesema amevunja maingiliano yote pamoja nao baada ya kwenda Yemen. Jirani mmoja anasema:

"Kijana huyu alikua jirani yetu aliyepitisha muda mrefu wa maisha yake nje ya Nigeria.Huko alichanganyika na watu ambao hajawahi kukutana nao maishani mwake.Ndio maana amebadilika.Unajua miezi sita iliyopita babaake mwenyewe alikwenda kwenye ubalozi wa Marekani na kulalamika dhidi ya msimamo wa mwanawe ambao ulikua wa kiajabu ajabu.Kwa hivyo ikiwa hata babaake ameingiwa na hofu seuze sisi majirani."

Al Qaida wamedai kuhusika na njama hiyo ya kutaka kuiripua ndege ya shirika la ndege la Marekani Delta.

Katika taarifa yao tawi la mtandao wa Al Qaida katika Raas ya Bara Arabu limesema walitaka kulipiza kisasi dhidi ya hujuma za Marekani dhidi ya wanaharakati wao nchini Yemen.

Yemen inachunguza kijana huyo wa kinigeria alikuwa na mawasiliano pamoja na nani alipokua nchini humo."Matukio ya uchunguzi huo yatakabidhiwa idara husika nchini Marekani-amesema hayo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Yemen mjini Sanaa.

Delta in Detroit - Terror - Northwest

Ndege ya shirika la ndege la Marekani Delta iliyosalimika na njama ya kutaka kuiripua

Nchini Marekani rais Barack Obama ameahidi nchi yake itawaandama mtindo mmoja magaidi wa itikadi kali,kokote kule wanakotokea.

Rais Barack Obama aliyezungumzia kwa mara ya kwanza kuhusu kisa hicho jana,ameapa wahusika watasakwa na watafikishwa mahakamani.

"Hatutochoka si mpaka tunawakamata wote wanaohusika,naiwe wanaotokea Afghanistan,Pakistan,Yemen au Somalia" amesema rais Obama akiwa likizoni Kaneohe Hawai.

Njama ya ijumaa ya Noel ya kutaka kuiripua ndege ya shirika la ndege la Marekani Delta,inawafanya watu wajiulize kuhusu hatua za usalama,viwanjani na ndani ya ndege-miaka minane baada ya mashambulio ya kigaidi ya september 11 mwaka 2001.

Rais Barack Obama ameitaka wizara ya usalama ijieleze imekwenda kwendaje mpaka mtu akaweza kuingia na miripuko hatari kama hiyo ndani ya ndege kutoka Amsterdam.

Kwa upande wake senetor Joe Liebermann amesema anapanga kuitisha kikao cha baraza la Congress kuzungumzia usalama ndani ya ndege.

Na huko Detroit,vyombo vya sheria vimesema mtuhumiwa atafikishwa mbele ya hakimu,january nane ijayo kusomewa mashtaka dhidi yake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Reuters,AFP)

Mhariri:Othman Miraji

 • Tarehe 29.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LG6u
 • Tarehe 29.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LG6u
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com