1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapanga kupunguza majeshi yake nchini Iraq

P.Martin - (RTRE/DPA)28 Februari 2009

Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza mpango wa kurejesha nyumbani sehemu kubwa ya vikosi vyake kutoka Iraq ifikapo mwezi wa Agosti mwaka 2010.

https://p.dw.com/p/H2w9
President Barack Obama speaks during a visit to Camp Lejeune, N.C., Friday, Feb. 27, 2009 as Defense Secretary Robert Gates, left, and Chairman of the Joint Chiefs Chairman Adm. Michael Mullen listen.. (AP Photo/Gerry Broome)
Rais Barack Obama akihutubia vikosi vya Marekani North Carolina, Ijumaa 27 Feb. 2009.Picha: AP

Kati ya wanajeshi 35,000 na 50,000 watabakia Iraq mpaka mwisho wa mwaka 2011 kutoa mafunzo na kusaidia vikosi vya usalama vya Iraq.Obama alifafanua mpango huo katika hotuba yake mbele ya wanajeshi wa Marekani huko North Carolina na kuongezea:

"Marekani itafuata mkakati mpya kumaliza vita vya Iraq kwa utaratibu wa mpito hadi Iraq itakapochukua jukumu kamili.Mkakati huo utatekeleza lengo la pamoja la Wairaki na Wamarekani- yaani kuwepo Iraq iliyo huru,tulivu na inayojitegemea."

Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iraq,Sharwan al-Waili vikosi vya nchi hiyo vimejiandaa kupokea mamlaka ya kusimamia usalama wa nchi majeshi ya Marekani yatakaporejea nyumbani.

Lengo la mpango huo wa Obama ni kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni ya uchaguzi kumaliza vita hivyo na kuimarisha operesheni za kijeshi nchini Afghanistan kumaaliza uasi wa wanamgambo nchini humo.

Rais wa Marekani amesema, eneo la Mashariki ya Kati litapewa kipaumbele katika enzi ya sera mpya za kidiplomasia za Marekani ikiwa ni pamoja na kufanywa majadiliano ya uso kwa uso na Syria na Iran.