1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Gibraltar kuendelea kuikamata meli ya Iran

Yusra Buwayhid
15 Agosti 2019

Wizara ya Sheria ya Marekani imetuma ombi la kuitaka meli ya Iran ya Grace 1 iendelee kushikiliwa nchini Gibtaltar kwa shutuma za kubeba mafuta na kuyapeleka nchini Syria hatua inayokiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3NyO1
Supertanker Grace 1 NEU
Picha: Getty Images/AFP/J. Guerrero

Marekani leo imeitaka Gibtaltar kuendelea kuishikilia meli ya mafuta ya Iran pamoja na kuikabidhi meli hiyo kwa maafisa wa Mareakani. Gazeti la Gibraltar Chronicles limeripoti kwamba ombi hilo la dakika ya mwisho, kutoka Wizara ya Sheria ya Marekani, limeisababisha Makahama Kuu ya Kusimamia eneo la ng'ambo la Uingereza kuchelewesha uamuzi wake kuhusu meli hiyo ya mafuta hadi baadaye leo. Hadi sasa hakuna maelezo zaidi kuhusu madai ya Marekani.

Soma zaidi: Uingereza, Iran zasaka muafaka meli ya mafuta

Msemaji wa serikali ya Gibraltar amesema nahodha wa meli hiyo pamoja na maafisa watatu wameachiliwa huru. Naye msemaji wa Rais wa Iran, Ali Rabiei, amekiambia kituo cha televisheni ya taifa kwamba hatua hiyo ya kukishikilia chombo cha Iran ilikuwa siyo sahihi, na kwamba wanatarajia mahakama ya Gibraltar itatoa uamuzi wa kuachiliwa kwake katika siku zijazo.

"Kukamatwa kwa meli ya mafuta ya Iran ilikuwa ni hatua isiyo sahihi tangu mwanzo, na tumekuwa tukitaka iachiliwe na tutaikaribisha hatua hiyo. Kwa kadiri ninavyojua, mahakama ya Gibraltar itaisikiliza kesi katika siku zijazo," amesema Rabiei.

Ali Rabiei erste Pressekonferenz
Msemaji wa wa rais wa Iran, Ali RabieiPicha: mehr

Mzozo wa kushikiliana meli

Mnamo Julai 4, makomando wa Jeshi la Majini la Uingereza, waliongoza operesheni ya kuikamata meli ya Iran kwa madai ya kwamba ilikuwa inakiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya vinavyozuia kusafirisha mafuta kwenda Syria. Kukamatwa kwa meli hiyo yenye uwezo wa kubeba mapipa milioni 2.1 ya mafuta ya Iran, pia kumepelekea kuongezeka kwa mivutano katika Ghuba ya Uajemi.

Wengi wa mabaharia wa meli hiyo walikuwa ni raia wa India na Pakistan. Maafisa wa Iran walidai kuachiliwa kwa meli hiyo mnamo Julai 5.

Soma zaidi: Meli ya mafuta ya Iran yakamatwa Gibraltar

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza katika taarifa yake kwamba kutekwa nyara kwa meli hiyo na serikali ya Uingereza ni hatua isiyokubalika.

Baadae mwezi huo huo wa Julai, Iran ilikamata meli mbili katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, moja iliyokuwa inapeperusha bendera ya Uingereza na ya pili ikiwa na bendera ya Liberia. Iran hadi sasa inazishikilia meli hizo.

Ombi la Alhamisi la Marekani linaweza kuwa kizuizi cha mataifa hayo hatimaye kubadilishana meli hizo ambazo kila upande imeshikila ya mwenziwe, ingawa hakuna makubaliano yoyote rasmi yaliyofikiwa hadi sasa.

Jaji Mkuu wa Gibraltar Anthony Dudley, amesema ingekuwa Marekani haikuingilia kati meli hiyo ikiruhusiwa kusafiri.