Marekani kusimamia mazungumzo kati ya Israel na Lebanon
10 Aprili 2026
Israel na Lebanon zitafanya mazungumzo mjini Washington wiki ijayo. Hayo yamesemwa na afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani jana Alhamisi, huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa kimataifa kwamba mashambulizi ya mabomu ya Israel yanaweza kuvunja mkataba wa kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran ambao tayari ni dhaifu.
Mapema Alhamisi waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliwaamuru mawaziri wake kutafuta mazungumzo ya moja kwa moja na Lebanon akishinikiza kupokonywa silaha kwa wanamgambo wa kundi la Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran.
Lakini afisa wa serikali ya Lebanon aliliambia shirika la habari la AFP kwamba Beirut ilihitaji makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya kuanza mazungumzo yoyote na Israeli.
Israel na Lebanon bado hazijathibitisha hadharani kuhusu mazungumzo ya Marekani.