1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Kongo na Rwanda kujadili amani ya DRC

Amina Abubakar Reuters, AP
17 Machi 2026

Marekani imewaita maafisa wakuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda kwa mkutano mjini Washington, kujadili mchakato uliokwama wa kutafuta amani ya Mashariki mwa DRC.

https://p.dw.com/p/5AXDZ
USA Washington D.C. 2025 | Trump, Kagame na Tshisekedi
Rais wa Rwanda Paul Kagame, Donald Trump wa Marekani na Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Kulingana na duru za kidiplomasia na msemaji wa ofisi ya rais nchini Kongo, Marekani itazungumza na kila mmoja hii leo Jumanne na baadae kesho Jumatano mkutano wa pande tatu utafanyika iwapo huu wa leo utafanikiwa kumalizika kwa amani. Haya yatakuwa mazungumzo ya kwanza kati ya pande hizo hasimu tangu Marekani ilipoliwekea jeshi la ulinzi la Rwanda RDF vikwazo pamoja na majenerali wake wanne mnamo Machi 2.

Washington mara zote imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoendelea kuzua vurugu Mashariki mwa DRC. Marekani ilisema jeshi hilo liliwaunga mkono waasi hao wanaohusishwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu mashariki mwa Kongo.

DR Kongo Goma 2025 | Corneille Nangaa
Kiongozi wa AFC/M23 Corneille NangaaPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani ilisema Rwanda iliwaunga mkono M23 wakati walipokuwa katika harakati za kuidhibiti miji miwili mikubwa ya Goma na Uvira pamoja na maeneo ya kimkakati ya uchimbaji madini. Wizara hiyo imesema hilo lisingewezekana bila ya uungaji mkono mkubwa kutoka kwa RDF. Rwanda imekuwa ikikanusha kuhusika kwa namna yoyote na kundi hilo la M23.

Mkutano una nafasi gani ya kufanikiwa?

Hata hivyo, wataalamu wanaelezea matumaini yao licha ya mkutano huo kufanyika baada ya Marekani kuiwekea Rwanda vikwazo. Lakini je safari hii mkutano huo una nafasi gani ya kufanikiwa? Ali Mali ni mchambuzi wa siasa za Afrika na mtaalam wa eneo la Maziwa Makuu, anasema: "Serikali ya Kongo inahitaji kufikia makubaliano ya amani, lakini serikali ya Rwanda haikubali makubaliano ya amani kwa kuridhiana na Kongo, bado na yenyewe ina masilahi yao. Kwahiyo utashi wa upatanishi ndio unaoweza kuleta pande hizi mbili  ziweze kukubali makubaliano iwe ni kwa kuridhia au kwa kinyongo."

Kongo na Rwanda: Nini kipo kwenye mkataba wa amani?

Mkutano huo wa Marekani na wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda,  unafanyika  wakati maafisa kadhaa wa serikali za Afrika wakikusanyika nchini Marekani kwa mkutano wa masuala ya miundombinu ya nishati na uwekezaji. Mkutano huo utawajumuisha mawaziri wa nishati kutoka sehemu mbali mbali ya bara la Afrika.