Marekani, China zatangaza mapatano kuhusu ushuru mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.12.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani, China zatangaza mapatano kuhusu ushuru mpya

China na Marekani zimeafikiana kutowekeana ushuru mpya wakati nchi hizo zikifanya majadiliano kwa lengo la kufikia makubaliano ndani ya siku 90. Makubaliano hayo yamefikiwa kati ya marais Donald Trump na Xi Jinping.

Trump alikubali kutopandisha ushuru kwa hadi asilimia 25 kwa bidhaa za China zenye thamani ya dola bilioni 200 ifikapo Januari Mosi kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali, baada ya China kukubali kununua kiwango kisichotajwa lakini "muhimu" cha bidhaa za kilimo, nishati, viwandani na nyingine, imesema ikulu ya White House.

Mapatano hayo, yaliyofikiwa baada ya karamu ya chakula cha usiku iliyodumu kwa zaidi ya masaa mawili, yanatoa muda kwa mataifa hayo mawili kushughulikia tafauti zao katika mzozo unaohusu kampeni ya ushari ya China kuchukuwa nafasi ya udhibiti wa Marekani wa nyanja ya teknolojia.

Ushindi kwa Trump?

"Ni makubaliano ya kushangaza," Trump aliwambia maripota kwenye ndege ya Air Force One. "Tutakachofanya ni kusitisha mpango wa kupandisha ushuru. China itazungumza, China itaondokana na ushuru. China itakuwa inanunua bidhaa nyingi kutoka kwetu," alisema Trump.

Xi Jinping und Donald Trump (Getty Images/T. Peter)

Rais wa Marekani Donald Trump akiteta jambo na Xi Jinping wa China.

Ikulu ya White House imesema pia kwamba China imeacha milango wazi kuweza kuidhinisha makubaliano ambayo hapo awali hayakuidhinishwa ya Qualcomm Inc NXP ikiwa yatalaazimika kuwasilishwa tena. 

Mwezi Julai, Qualcomm - mtengenezaji mkubwa kabisa duniani wa vifaa vya kuhifadhi data katika simu za kisasa za 'smartphone' iliachana na mpango wa  dola bilioni 44 wa ununuzi wa vipitishi vya umeme kutoka NXP, baada ya kushindwa kupata idhini ya mamlaka ya udhibiti ya China, na kuwa mwathirika wa ngazi ya juu wa mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani.

Imesema ikiwa makubaliano kuhusu masuala ya biashara, ikiwemo uhamishaji wa teknolojia, hataza, vikwazo visivyo vya kodi, wizi wa mtandaoni na kilimo hayajafikiwa na China katika kipindi cha siku 90, kwamba pande zote mbili zinakubaliana kwamba ushuru wa asilimia 10 utapandishwa kwa hadi asilimia 25.

Trump aliweka ushuru wa asilimia  10 kwa bidhaa za thamani ya dola bilioni 200 kutoka China mwezi Septemba. China ilijibu kwa kuweka ushuru wake. Trump pia ametishia kuongeza ushuru kwa bidhaa nyingine za China zenye thamani ya dola bilioni 267.

'Ishara nzuri ya kiutu'

Ikulu ya White House ilisema Xi, "katika ishara nzuri ya kiutu," alikubali kuianisha dawa ya usanisiya ya fentanyl kama dawa inayodhibitiwa, na hivyo kufanya uuzwaji wake nchini Marekani kutegemea adhabu kubwa kabisa ya kisheria nchini China. Dawa nyingi zaidi zinazoingizwa nchini Marekani zinatengenezwa China.

Symbolbild USA-China-Handelskrieg (Colourbox)

Mzozo wa kibiashara kati ya China na Marekani imesababisha wasiwasi wa kiuchumi duniani.

China pia imekubali kuanza kununua bidhaa za kilimo kutoka kwa wakulima wa Marekani mara moja, kwa mujibu wa ikulu ya White House.

Kampuni za Marekani na watumiaji wanabeba sehemu ya gharama na ushuru wa Marekani kwa China, kwa kulipia bei kubwa kwa bidhaa, na kampuni nyingi zimepandisha bei za bidhaa za nje.

Na wakati huo huo, wakulima wa Marekani wameumizwa na hatua ya China kupunguza manunuzi ya maharage ya soya na bidhaa nyingine.

Rais Trump amesifu mkutano wake na rais Xi na kuutaja kuwa wenye ufanisi uliojitokeza na fursa zisizo na mipaka kwa mataifa yote mawili, na kwamba ilikuwa "heshima kubwa" kufanya kazi na Xi.

Mkutano huo ndiyo ulikuwa tukio muhimu zaidi la ziara ya Trump ya siku mbili nchini Argentina alikohudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa yanayoongoza kiuchumi duniani G-20, baada ya rais huyo kufuta mkutano wake na Rais wa Urusi Vladmir Putin kuhusiana na mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, afpe

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com