Mapinduzi ya Kijeshi Niger. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Mapinduzi ya Kijeshi Niger.

Utawala mpya wa Kijeshi wa Niger, umeimarisha ulinzi, kwa kutumia vifaru na magari ya kijeshi, katika makaazi ya Rais aliyepinduliwa madarakani, Mamadou Tandja, siku moja tu, baada ya jeshi la nchi hiyo kufanya mapinduzi

Rais Mamadou Tandja wa Niger, ambaye ameondolewa madarakani, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea jana nchini humo.

Rais Mamadou Tandja wa Niger, ambaye ameondolewa madarakani, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea jana nchini humo.

Wakati jeshi likiimarisha ulinzi katika makaazi ya Rais, Umoja wa Afrika umelaani mapinduzi hayo yaliyofanywa nchini humo, baada ya Jeshi kutangaza kudhibiti nchi.

Jean Ping ayalaani mapinduzi ya Niger: Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika leo imesema Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo, Jean Ping, ameshutuma mabadiliko ya serikali yaliyofanywa kinyume na katiba ya nchi hiyo, pamoja na mapinduzi hayo ya kijeshi.

Pia amearifu kuwa anafuatilia kwa karibu na kwa wasiwasi hali inavyoendelea nchini Niger.

Katika taarifa iliyotolewa na Umoja Afrika, Bwana Ping amekuwa akiwasiliana na Rais wa Jumuia ya Kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS, pamoja na wahusika wengine wanaoushughulikia mzozo huo.

Bwana Ping ameitaka nchi hiyo haraka kufuata katiba.

Mapema usiku wa kuamkia leo, serikali mpya ya Niger ilitangaza kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo, siku moja tu baada ya kufanyika mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Mamadou Tandja.

Hali shwari kwa sasa: Aidha doria ndogo ya jeshi leo pia imekuwa ikiendelea katikati ya mji mkuu wa Niger, huku shughuli za kibiashara zikiendelea kama kawaida na shule kufunguliwa,

Baadhi ya maeneo ya mji huo yamearifiwa kuwa kimya baada ya tangazo hilo lililotolewa jana la watu kutotembea usiku.

Niger Wahlen

Miongoni mwa Wakaazi wa Niger.

Mbali na magari ya kijeshi kupiga doria katika makazi ya Rais, ulinzi huo umeimarishwa pia mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya nje ya nchi hiyo.

Utawala wa kijeshi nchini humo unaojiita Baraza kuu la Kurejesha Demokrasia, ambalo kiongozi wake anajulikana kwa jina la Salou Djibo, jana ulimkamata Rais Tandja na mawaziri wake katika mapigano yaliyodumu saa nne, kabla ya kuisitisha katiba ya nchi hiyo na kuzivunja taasisi zote za serikali.

Watu watatu walikufa katika mapigano hayo.

Hata hivyo, utawala huo wa kijeshi, ambao unaonesha kuungwa mkono na raia wengi wa nchi hiyo waliokatishwa tamaa na serikali iliyopinduliwa, haukutoa ishara zozote kwamba ni kwa muda gani utashikilia madaraka, lakini uliahidi kuwa utamaliza hali tete ya kisiasa nchini humo, na kuiunga mkono jumuiya ya kimataifa..

Mbali na Umoja wa Afrika kutoa kauli yake, Jumuia ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS , imesema pia itaiadhibu hatua yeyote ya kutwaa madaraka kinyume na katiba..

Lakini hata hivyo, kwa upande wao wanademokrasia wameashiria kuwa mapinduzi hayo yanaweza kutoa mwanzo mpya na kufungua milango ya kufanyika uchaguzi.

Mwandishi: Halima nyanza(Reuters,ap,afp)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 19.02.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M5Zq
 • Tarehe 19.02.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M5Zq
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com