1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesha makubwa zaidi ya kiviwanda yafunguliwa mjini Hanover

Maja Dreyer16 Aprili 2007

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliyafungua rasmi maonyesho ya kiviwanda ya Hanover, ambayo ni moja kati ya maonyesho makubwa zaidi ya kiviwanda duniani. Yule ambaye anataka kujua kuna teknolojia gani mpya za kiviwanda, lazima aende Hanover wiki hii.

https://p.dw.com/p/CHlD
Teknolojia ya kisasa kabisa kwenye maonyesho ya Hanover
Teknolojia ya kisasa kabisa kwenye maonyesho ya HanoverPicha: AP

Hadi leo asubuhi, mafundi walikuwa na kazi chungu nzima ya kujenga mabanda ya makampuni yanayoonyesha bidhaa na teknolojia zao huko mjini Hanover. Kila kitu kilikuwa tayari kwa ufunguzi wa maonyesho ya Hanover kwa wageni. Kwa ujumla, makampuni 6400 kutoka nchi 60 yanajionyesha mjini Hanover, yaani makampuni 1400 zaidi ukilinganisha na mwaka jana. Hii ni ishara ya hali ya uchumi kuboreka sana baada miaka kadhaa ya maonyesho ya Hanover kupoteza umuhimu wake. Sasa lakini mafanikio ni kama yale ya miaka 60 iliyopita, pale maonyesho yalipofanyika mara ya kwanza.

Katika muda huo wote, maonyesho ya Hanover yalikuwa kama kipimo cha hali ya uchumi, kama anavyosema Ulrich Koch wa shirika la maonyesho ya Ujerumani: “Katika miaka miwili, mitatu iliyopita ilitubidi kufanya marekebisho kuhusiana na masuala fulani, yaani kushughulikia masuala ambayo ni muhimu siku hizi. Hii pamoja na kuwa na hali nzuri ya uchumi humu nchini na ulimwenguni kwa ujumla ilisaidia maonyesho haya yachukue nafasi ya kwanza kama ilivyokuwa zamani.”

Masuala yanayopewa kipaumbele mwaka huu ni utumiaji wa mitambo inayojiendesha katika viwanda pamoja na suala la nishati. Nafasi nyingi ya maonyesho haya inachukuliwa na makampuni yanayoonyesha teknolojia mpya ya kutengeza nishati na ya kupunguza matumizi ya nishati.

Kama kawaida, nchi moja ni nchi ya ushirikiano maalum ya maonyesho ya Hanover, mwaka huu ikiwa ni Uturuki. Kwa hivyo, Kansela Merkel, katika kuyafungua rasmi maonyesho hayo, alisindikizwa na waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan. Kwenye sherehe hiyo, Angela Merkel alisema: ushirikiano huu kati ya Ujerumani na Uturuki unaonyesha vile nchi hizo mbili zina mahusiano mazuri ya kiuchumi. Lakini pia, Kansela Merkel alisisitiza ushirikano wa kisiasa: “Tukizingatia jinsi tunavyozungumzia wazi masuala magumu kati nchi yetu, basi naona kuwa njia ya ushirikiano na uhusiano wa kirafiki inapaswa kuendelea vizuri katika mahusiano baina ya Ujerumani na Uturuki, si tu katika sekta ya uchumi.”

Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, alikumbusha tena lengo la Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya akisisitiza ukuaji wa uchumi nchini mwake. Kabla ya ziara yake nchini Ujerumani, Erdogan aliikosoa Ujerumani kwa kutofanya bidii ya kutosha kuhusiana na uwanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya. Ukosoaji huo lakini hajaukariri mjini Hanover.