Magazetini.
16 Septemba 2008Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya mgogoro mwingine wa fedha uliosababishwa na benki ya vitega uchumi, Lehmann Brothers nchini Marekani.
Lakini wahariri hao pia wanazungumzia juu ya makubaliano ya kugawana mamlaka yaliyofikiwa baina ya rais Robert Mugabe na mpinzani wake mkuu Morgan Tsvangirai nchini Zimbabwe. Gazeti la Passauer Neue Presse linasema makubaliano hayo maana yake ni mwisho wa damu kumwagika nchini Zimbabwe.
Kuhusu mgogoro mwingine wa fedha uliosababishwa na benki ya vitega uchumi Lehmann Brothers ya Marekani gazeti la Berliner Zeitung linaonya dhidi ya serikali kuingilia kati na kujaribu kuyasaidia mabenki ama mashirika ya fedha yanayokabiliwa na matatizo.
Mhariri wa gazeti la Berliner Zeitung anakumbusha historia ndefu ya benki ya Lehman Brothers, iliyoweza kuhimili misukosuko ya vita kuu mbili,na mgogoro wa uchumi wa miaka ya 30. Lakini licha ya kuweza kuhimili misukosuko hiyo mikubwa katika historia yake ndefu, benki hiyo ,huenda ikatoeka. Mhariri anasema waliokuwa wanafikiria kuisaidia benki hiyo sasa wametambua kwamba msaada wa serikali usingelikuwa na manufaa.
Mhariri wa gazeti la Der neue Tag anaunga mkono maoni ya gazeti la Berliner Zeitung kwa kukariri usemi unaosema kuwa hakuna mwenye ukubwa wa kuweza kuhimili misukosuko yote.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa sasa umefika wakati wa kuachana kabisa na tabia ya kibinafsisha mapato makubwa yanayotokana na biashara za mashaka, lakini wakati huo huo kutumia fedha za walipa kodi kufidia hasara zinapotokea.
Mhariri wa gazeti la Nordsee anasema
,mzigo siku zote unabebwa na wateja,
wadogo wadogo, pamoja na walipakodi.
Gazeti linafafanua kwa kusema kwamba walipa kodi na wateja wenye akaunti katika benki wanabeba mizigo inayotakana na migogoro ya fedha kwa sababu , mabenki na mashirika yote ya fedha yameungana katika mtandao kutokana na mfumo wa dunia utandawazi. Gazeti linasema kutokana na mfumo huo, watu wote wanaathirika. Gazeti linasema hayo yataonekana katika siku za usoni baada ya akaunti za watu kuteketea.
Lakini mhariri wa gazeti la Fränkischer Tag anasema hakuna haja ya kuwa na kiherehere nchini Ujerumani.
Gazeti linasema mfumo wa fedha wa Ujerumani ni imara sana, na kwa hiyo hakuna haja ya mtu kuwa na wasiwasi.