Magazetini.
22 Julai 2008Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wameandika kwa mapana na marefu juu ya seneta wa Illinois Barack Obama anaegombea kiti cha urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha demokratik. Obama anatarajiwa kuanza ziara alhamisi ijayo nchini Ujerumani.
Lakini wahariri wengine hawajasahau
suala linalowahusu zaidi wajerumani
wote- yaani uchumi wa nchi. Baadhi
wanasema uchumi wa Ujerumani
unaonesha dalili za kuanza kurudi
nyuma.
Juu ya seneta Barack Obama,
gazeti la Der neue Tag linasema theluthi mbili ya Wajerumani wangelimpigia kura Obama. Ni asilimia 10 tu ya wajerumani wangelimpa kura zao mshindani wake John McCain. Lakini mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba uchaguzi unafanyika Marekani na siyo nchini Ujerumani. Ndiyo kusema haiwezekani kumpuuza John McCain.
Lakini mhariri wa gazeti la Kölnische Rundschau anasema angalau, Obama anatambua changamoto za nyakati za sasa.
Gazeti hilo linaeleza kuwa uwanja wa mapambano dhidi ya magaidi wa Alkaida upo katika maeneo ya Hindukush kwenye mpaka na Pakistan. Obama ametambua hayo.
Lakini gazeti linasema ,ni vigumu kuwasilisha ukweli huo kwa utawala wa Bush.
Gazeti la Bild Zeitung linazungumzia juu ya uchumi wa Ujerumani, na linasema kuwa ishara zilizopo juu ya uchumi huo siyo nzuri.
Gazeti linasema masoko ya hisa yanaserereka, bei ya mafuta inaongezeka na sasa zinafuatia vurumai za uchumi wa dunia zinazoathiri uchumi wa Ujerumani. Mhariri anasema pamoja na hayo yote uchumi wa Ujerumani bado unaonesha maajabu. Lakini, kuanzia mwaka kesho hali itakuwa nyingine. Ishara zinaonesha kuwa ustawi utanywea. Mawingu yanaaashiria kuwa patakuwa na dhoruba mwakani, katika uchumi wa Ujerumani.
Gazeti la Badische Zeitung nalo linasisitiza kuwa,athari za kurudi nyuma ustawi wa uchumi wa Ujerumani zitaonekana katika soko la ajira.
Mhariri wa gazeti hilo anasema huenda idadi ya wasiokuwa na ajira ikaongezeka nchini Ujerumani.Ishara juu ya uwezekano huo zinaongezeka.