Magazeti ya Ujerumani.
21 Mei 2008
Mpango wa kuongeza mishahara ya wabunge nchini Ujerumani umeachiliwa mbali. Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya hapa nchini wanazungumzia juu ya uamuzi huo.
Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya kushambuliwa na kuuliwa wageni hasa waafrika, nchini Afrika kusini.
Juu ya uamuzi wa kuacha mpango wa kuongeza mishahara ya wabunge gazeti la Neue Osnabrücke linasema wabunge lazima wazingatie maoni ya wananchi. Kila mbunge anapaswa kuwajibika kwa wapiga kura wake- anapaswa kueleza kwa nini anastahili kuongezewa mshahara.
Gazeti hilo linaeleza kuwa uamuzi wa
kughairi mpango huo pia unatokana na
kutambua kwamba wapo wananchi
wengi wenye hali mbaya.
Lakini gazeti la Nürnberger Nachrichten linasema uamuzi huo unaonesha kwamba bunge la Ujerumani halina ujasiri. Gazeti linasema, ndio wabunge wanastahili kulipwa vizuri lakini waache tabia ya kuvuka mipaka inapohusu kujihakikishia malipo ya uzeeni.
Gazeti la Financial Times Deutschland linasema katika maoni yake kuwa licha ya kuamua kuacha mpango wa kuwaongezea wabunge mishahara, wabunge hao hawataweza kukwepa shutuma za wananchi.Wananchi wanawaona wabunge hao kuwa watu wenye uchu wa fedha.
Hatahivyo mhariri anasema utaratibu wa wabunge kuongezewa mishahara kila baada ya muda fulani bado upo palepale. Ndiyo sababu kuwa pana haja ya kutafuta njia nyingine.
Gazeti la Berliner Zeitung linazungumzia juu ya matukio ya kusikitisha nchini Afrika Kusini ambapo raia wa kigeni wanashambuliwa na kuuliwa.
Gazeti hilo linasema katika maoni yake kuwa kufumuka kwa ukatili dhidi ya wageni siyo jambo la kushangaza. Gazeti linasema hali hiyo inatokana na msongamano wa matatizo ya muda mrefu nchini humo.
Mhariri anaeleza kuwa, uchumi wa nchi unastawi na kunawiri,lakini wananchi wengi hawaambulii kitu.
Kutokana na kutamauka, maalfu ya wazalendo wanaelekeza ghadhabu zao kwa wageni. Na gazeti la Döbelner Anzeige linasema ,kinachotokea Afrika Kusini ni aibu kubwa , hasa kwa kutambua kwamba ,kwa karne nyingi waafrika walikandamizwa chini ya mfumo wa kibaguzi -apartheid.