Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 16.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani bwana Wolfgand Schäuble anaamini kuwa Ujerumani ni miongoni mwa nchi zenye usalama mkubwa licha ya hatari ya ugaidi. Lakini Polisi ya nchi hii ina maoni tofauti juu ya hayo. Baadhi ya wahariri wa magazeti wanakubaliana na hayo.

Ripoti ya serikali juu ya hali ya usalama hapa nchini inahitilafiana na tathmini ya polisi. Mhariri wa gazeti la LANDSHUTTER anatilia maanani katika maoni yake kuwa wakati waziri wa mambo ya ndani bwana Wolfgang Schäuble anaamini kwamba Ujerumani ina usalama mkubwa licha ya hatari ya ugaidi , idara ya polisi ina maoni tofauti.

Idara ya polisi inajua inachozungumza kwani polisi ndiyo wanaokabiliana na hali halisi ya kila siku linasema gazeti hilo . Idara hiyo inalalamika, kwa mfano kwamba vyama vya siasa havina mkakati wowote juu ya kukabiliana na hatari ya makundi ya mafashisti mamboleo hapa nchini. Idara hiyo inasema hadi sasa Ujerumani imebahatika kuponyoka hatari ya waislamu wenye siasa kali na makundi ya watu wanaoshirikiana na magaidi.

Mhariri wa gazeti la MAIN ECHO anasema kuwa idara za serikali zimekuwa zinaelekeza makini yote katika kukabiliana na tishio la ugaidi na kusahau kazi za kila siku zinazofanywa na polisi .

Mhariri huyo anauliza ,jee pana faida gani , ikiwa Ujerumani kweli haikabiliwi na hatari ya mashambulio ya kigaidi, lakini mwananchi wa kawaida anaogopa kutoka nyumbani kwake saa za jioni?

Hatahivyo mhariri wa gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG anasema kuwa kulinganisha na nchi zingine hali ya usalama ni nzuri zaidi nchini Ujerumani.

Anasema ni kweli kwamba si jambo rahisi kwa mtu kuondoka nyumbani kwake saa za usiku: wakaazi wa miji kadhaa ya Ufaransa kwa mfano hawawezi kutoka nje ya nyumba zao saa za usiku.

Wakaazi wa mji wa Neaple wangelifurahi kama wangeliweza kuishi kama wanzao nchini Ujerumani.

Lakini gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba baadhi ya wakaazi wenye nasaba za kigeni wanaishi wakiwa na hofu katika baadhi ya miji nchini Ujerumani.

Lakini kutokana na kazi nzuri ya polisi na idara za sheria hali ya usalama ni nzuri kwa watu hao.

Gazeti la NEUEN WESTFÄLLISCHEN kutoka mji wa Bielefeld linazungumzia juu ya wazo la kuwapa kibali wageni ambao wamekuwa wanaishi nchini Ujerumani kinyume cha sheria.

Watu karibu 190,000 wapo katika kundi hilo. Jee itakuwa sawa kuhalalisha uwepo wa watu hao?. Mawaziri wa mambo ya ndani wa majimbo ya Ujerumani leo wanakutana kuzungumzia suala hilo.

Mhariri wa gazeti hilo anasema mtu yeyote ambae ameishi kwa muda mrefu hapa nchini, kwa kuheshimu sheria, na ikiwa anataka kuwa mwananchi , anastahili kupewa fursa hiyo. Usikizano uliofikiwa miongoni mwa viongozi wa serikali juu ya kuwapa watu hao uwezekano wa kuendelea kuishi nchini ,ni muhimu na sahihi anasema mhariri huyo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com