Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 11.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri

Kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Irak Jenerali Petraeus ametoa taarifa juu ya hali ya usalama nchini humo wakati ambapo Marekani inakumbuka mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika miaka sita iliyopita nchini humo. Hayo ndiyo yanayozungumziwa na wahariri leo.

Katika maoni yake mhariri wa gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER anatilia maanani kwamba idadi ya askari wa Marekani waliouawa nchini Irak hadi sasa inavuka ile ya watu walioangamizwa katika mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika tarehe kama ya leo miaka sita iliyopita nchini Marekani kwenyewe.

Mhariri huyo anauliza iwapo hatua ya Marekani kuingia Irak kijeshi ilikuwa sahihi na iwapo imeleta malipo yaliyokusudiwa.Mhariri huyo anaendelea kuuliza iwapo ilikuwa hatua mujarabu kuanzisha mashambulio ya kijeshi ili kujibu waliyotenda magaidi miaka sita iliyopita.

Gazeti linasema hiyo ndiyo sababu kwamba watu nchini Marekani walisubiri kwa hamu kusikia ushauri wa busara kutoka kwa jenerali Petraeus kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Irak.Mhariri huyo anatamka kuwa yaliyotokea nchini Marekani miaka sita iliyopita ni historia lakini vita vya nchini Irak bado vipo.

Gazeti la mjiniLÜNEBURG,LANDESZEITUNG linamshauri jenerali David Petraeus aombe muda zaidi kutoka kwa bunge la Marekani kabla ya kufanya pupa ya kuondoa majeshi .

Mhariri wa gazeti hilo kutoka jimbo la Lower Saxony kaskazini magharibi mwa Ujerumani anasema haitakuwa sawa asilani kufanya pupa katika kuondoa majeshi ya Marekani kutoka Irak. Anasema mbio kama zile za mwaka 1975 kutoka Saigon Vietnam zitaitumbukiza Irak na eneo lote la mashariki kati katika vurumai kubwa.

Na mhariri wa gazeti la mjini Berlin, NEUES DEUTSCHLAND anaeleza katika maoni yake kwamba alichopendekeza jenerali Petraeus ni kuchelewesha maamuzi.Anatilia maanani kuwa hicho hasa ndicho wanachotaka wajumbe wa chama cha demokratik ili waweze kujijengea hoja za kushinda katika uchaguzi wa rais.

Gazeti linasema kuwa ,hadharani wajumbe wa chama cha Demokratik wanazungumzia juu ya kuondolewa haraka majeshi ya Marekani kutoka Irak, lakini pembe za chaki wanatambua kwamba ngwe ya kukatuliwa nchini Irak bado ni ndefu.

Hayo pia anayesema mhariri wa gazeti la Esslinger.Anaeleza kuwa wajumbe wa chama cha Demokratik wamekuwa wanatumia maneno makali dhidi ya rais Bush. Lakini wao pia wanahofia mauaji halaiki yanayoweza kutokea nchini Irak ikiwa Marekani itaondoa majeshi kwa njia za pupa.

.