1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Putin

Abdu Said Mtullya18 Machi 2014

Wahariri karibu wote wanauliza, iwapo vikwazo vilivyotangazwa na nchi za Magharibi dhidi ya Rais Putin vitaiathiri Urusi, au ni maji ya moto tu yasiyounguza nyumba?

https://p.dw.com/p/1BRP8
Rais Wladimir Putin wa Urusi
Rais Wladimir Putin wa UrusiPicha: picture-alliance/dpa

Mhariri wa gazeti la "Rhein" amekiri kwamba vikwazo vilivyotangazwa na nchi za Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi ni sawa na kumfinya mtu tu. Hata hivyo,mhariri huyo ameeleza kuwa, uzito wa vikwazo hivyo upo katika ujumbe unaowasilishwa kwa Rais Putin kwamba huenda hatua nyingine zikafuatia.

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linasema katika maoni yake kwamba hatua zilizochukuliwa na nchi za Umoja wa Ulaya dhidi ya Rais Putin zinaonekana kama ni za kutapatapa.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kuwazuia watu 21 kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya na kuzizuia akaunti za benki za watu fulani, siyo hatua inayoonyesha msimamo thabiti katika kumwadhibu Putin kutokana na kufanyika kwa kura ya maoni katika muktadha wa vitisho vya kijeshi katika jimbo la Krimea. Hata hivyo, vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za Umoja wa Ulaya ni ishara kwamba Umoja huo haukubaliani na hatua ya Rais Putin.

Gazeti la "Leipziger Volskzeitung" linauliza iwapo palikuwa na haja hata kidogo, kwa Umoja wa Ulaya kuviweka vikwazo hivyo ikiwa mbunge wa Bunge la Ulaya, Bwana Elmar Brok, amesema kuwa sasa wake wa matajiri wa Urusi hawataweza tena kuenda London ili kununua mahitaji yao. Mhariri huyo anasema ikiwa hilo ndilo lengo la vikwazo, basi Umoja wa Ulaya utapaswa utafute shughuli nyingine ya kuifanya.

Uchaguzi wa Serbia

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linazungumzia juu ya matokeo ya uchaguzi nchini Serbia. Linasema Bwana Vucic ameshinda katika uchaguzi huo kwa kura nyingi. Sasa yeye ni Waziri Mkuu mpya wa Serbia. Ndiyo kusema anapaswa kuyaleta mageuzi aliyoahidi tokea miaka 2 iliyopita, ikiwa pamoja na kupambana na rushwa na kuyatenganisha mahakama na dola. Mazungumzo juu ya Serbia kujiunga na moja wa Ulaya yanamsubiri Waziri mkuu huyo mpya, Bwana Vucic .

Mashindano ya silaha

Gazeti la "Freie Presse" linalotoa maoni juu ya ripoti ya shirika la Sipri juu ya mashindano ya silaha. Mhariri wa gazeti hilo anasema mashindano hayo yanasababisha hatari kubwa katika bara la Asia hasa kutokana na migororo ya kikabila, kidini na mingine ya kihistoria. India na Pakistan zinazidi kuekeza katika sekta ya kijeshi na ununuzi wa silaha. Sera hiyo inaligeuza bara la Asia kuwa pipa la baruti.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef