Maoni ya wahariri juu ya janga la moto | Magazetini | DW | 27.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya janga la moto

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya maafa ya moto yaliyotokea kusini magharibi mwa Ujerumani na kusababisha vifo vya watu 14.

Janga la moto katika mji wa Neustadt

Janga la moto katika mji wa Neustadt

Gazeti la "Osnabrücker linafungua na maoni juu ya maafa yaliyotokea katika mji wa Neustadt kusini magharibi mwa Ujerumani.Watu 14 walikufa jana baada ya moto kuzuka katika nyumba ya walemavu. Mhariri wa gazeti hilo anauliza jee ingeliwezekana kuliepusha janga hilo?Anaeleza. Mjadala wa siku zinazofuatia tayari unajulikana. Jee ni nini hasa kilichosababisha moto huo kuzuka?Na jee ingeliwezekena kuuepusha? Jee taratibu za usalama zinatosha kwenye nyumba ya walemavu ambako moto ulitokea.?Yumkini patatokea mjadala mkali juu ya nani anabeba lawama. Lakini jambo moja ni wazi, kwamba jamii imevunja ahadi iliyotoa juu ya kuwahudumia wale wanaohitaji kuangaliwa-walemavu.

Mhariri wa gazeti la "Schwarzwälder Bote" anaitaka jamii isimame mstari wa mbele katika kuhakikisha usalama wa watu wanaohudumiwa kwenye nyumba za walemavu.Na anasema kwamba maafa yaliyotokea jana,kusini magharibi mwa Ujerumani yamesababisha mshtuko, butaa na fadhaa. Hapo awali jamii ilizungumzia juu ya usalama kwenye nyumba za walemavu ingawa kwa kweli mtu asingependelea sana kulisikia neno hilo- la kuwalinda walemavu. Sababu ni kwamba watu wenye ulemavu hawapendelei kuwekwa katika fungu maalumu.Lakini ukweli ni kwamba watu hao wanahitaji kuhakikishiwa usalama kwa kadri itakavyowezekana.Na hiyo ndiyo sababu kwamba pana ulazima wa kukichunguza chanzo kilichosababisha maafa.

Gazeti la "Braunschweiger" linazungumzia juu ya mkutano wa mjini Doha ambako wajumbe zaidi ya alfu 20 kutoka duniani kote wanajadili mabadiliko ya hali ya hewa-tabia nchi.Katika maoni yake mhariri wa gazeti hilo anasema njia ya kuelekea katika mabadiliko ya sera ya tabia nchi bado haijakaa vizuri.Mhariri huyo anafafanua kwamba Marekani inasuasua inapohusu kuchukua hatua zaidi za kupunguza utoaji wa gesi inayoharibu mazingira.Badala yake inainyooshea kidole China inayotoa asilimia 25 ya gesi chafu. Na kwa upande wake China inazitaka nchi za viwanda zikubali wajibu wa kuongoza katika kupunguza utoaji wa gesi chafu. Na kwa hivyo mchezo wa kutupiana lawama unaendelea.Tukae tukijua kwamba, tukiendelea na mchezo huo,hivi karibuni tu mambo yataenda mrama kabisa.

Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya na wajumbe wa shirika la fedha la kimataifa,IMF wamefikia mapatano ya kuipa Ugiriki msaada mwingine wa fedha ili kuikoa nchi hiyo iliyotingwa na madeni.Lakini mhariri wa gazeti la "Der neue Tag"anasema safari haijaishia hapo.Na anaeleza kuwa safari hiyo hatimaye itaishia katika kuifutia nchi hiyo deni lake.Hatima hiyo haiwezi kuepukwa.Swali sasa siyo ni,iwapo Ugiriki itafutiwa deni laki, bali ni lini deni hilo litafutwa.

Mwandishi:Mtullya abdu.Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Abdul-Rahman