Manu leo bila ya Wayne Rooney dhidi ya Chelsea | Michezo | DW | 02.04.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Manu leo bila ya Wayne Rooney dhidi ya Chelsea

Kombe la Afrika larudi uwanjani na TP Mazembe.

default

Manu bila ya Rooney itatamba ?

Mabingwa wa kombe la klabu bingwa barani Afrika TP Mazembe na mabingwa mara 6 Al Ahly ya Misri ,wana azma mwishoni mwa wiki hii kufuta madhambi ya duru iliopita waliofanya kwa APR ya Rwanda na Gunners ya Zimbabwe.

Baada ya Bayern Munich , kutamba champions-league mbele ya Manchester united kwa mabao 2-1, leo (Jumamosi) ina miadi na Schalke katika changamoto ya timu ya kwanza na ya pili kileleni mwa Bundesliga.

Huko Uingereza pia -asie na mguu atie gongo-mkutano uwanjani "Old Traford": Manchester United bila ya Wayne Rooney, inaonyeshana na Chelsea nani bingwa kuliko mwenziwe :

Mabingwa wa Afrika TP Mazembe , kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ,walifanya uzembe duru iliopita pale waliporejeshwa nyumbani Lumbubashi, na bao 1 kikapuni na Jeshi la Rwanda, APR huko Kigali.

APR , ni timu yenye maarifa makubwa ya kuhimili vishindo katika kinyan'ganyiro hiki .Lakini, pirika-pirika zao kuwasili duru ya kutoana ya Kombe hili kwa mara ya kwanza, huenda zikashia kambini mwao Kigali, ingawa APR imesajili mastadi wengi wapya msimu huu.

Mabingwa mara 6 Al Ahly, ya Misri, wanapigiwa debe kutamba mbele ya Gunners -timu iliopanda daraja ya kwanza ya ligi ya Zimbabwe miaka 2 tu iliopita.Ikitamba Al Ahly nyumbani , itasonga mbele duru ya 3 licha ya kulazwa duru iliopita mjini Harare.

Mabingwa wa zamani wa Kombe hili ASEC Mimosa ya Ivory Coast, wana kibarua cha kufuta bao 1 la mabingwa wa Zambia, ZANACO kutoka duru ya kwanza kesho katika Uwanja wa Felix Houphouet -Boigny.Huko Oweri,Nigeria, Heartland FC, inaikaribisha Tiko united, mabingwa wa Kameroun baada ya timu hizo mbili, kumalizana sare 2:2 wiki 2 zilizopita.

Huku Ulaya, mashabiki wanatega sikio na wengine, wanazikodolea macho Ligi 2: Bundesliga kwa mpambano kati ya Bayern Munich iliopo nafasi ya pili na Schalke inayoongoza Ligi nafasi ya kwanza.Nani mwishoe, atachukua usuakani wa ligi hii leo ? Katika Premier league huko Uingereza kuna zahama leo baina ya Manu na Chelsea:

Schalke haikulazwa nyumbani tangu Septemba mwaka jana wakati Munich, iliaibishwa nyumbani Jumamosi iliopita na Stuttgart kabla miadi yao na Manu.

Leverkusen, iliopo nafasi ya 3 wana miadi na Frankfurt ambayo iko pointi 3 tu nyuma ya Hamburg ilioangukia nafasi ya 6.Dortmund inaikaribisha leo Bremen , inayoania tiketi ya mwisho ya kucheza mwakani kombe la Champions league.Stuttgart iliotamba mbele ya Bayern Munich, mwishoni mwa juma lililopita, ina vita leo na Borussia Moenchengladbach kuania pointi 3.

Mkiani mwa Bundesliga, Hertha Berlin, itataka pointi zote 3 kesho Jumapili kutoka kwa wenyeji wao FC Cologene, ambao watakuwa na uchu kuonesha ukarimu kwavile, wao pia, wanazihitaji ili kubakia daraja ya kwanza msimu ujao.Kesho kalenda itakamilishwa na Wolfsburg na Hoffenheim wakati majirani 2 Hamburg na Hannover, wataania pointi 3 za mwisho .

Bila ya mzinga wao mjarabu,Wayne Rooney, alieumia majuzi pale Manu ilipochezeshwa kindumbwe-ndumbwe sekunde ya mwisho na Bayern Munich,Manchester United ina miadi leo na Chelsea.Nani atatamba leo ?Je, bila Rooney, Berbetev, atatosha kuinusuru Manu Old Traford ?

Arsenal iliomudu sare ya mabao 2:2 na FC Barcelona, katika champions league kati ya wiki, iko nyumbani ikiikaribisha Wolverhampton Wanderes.Liverpool itakuwa kesho uwanjani kwa miadi yake na Birmingham wakati Fuilham, iliotamba katika Kombe la ulaya la Ligi dhidi ya mabingwa wa Ujerumani Wolfsburg hapo juzi,itakutana kesho na Wigan Athletic huku Everton wakicheza na West Ham.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE

Uhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com