1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malori yaliyobeba mahindi yakwama mpakani Namanga

Veronica Natalis9 Machi 2021

Hali ya biashara katika mpaka wa Namanga unaziunganisha nchi za Kenya na Tanzania imezorota kutokana na msururu wa magari makubwa ya kubeba mahindi kutoka Tanzania kuzuiwa kuingia nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/3qOcX
Tansania Arusha | Mais Transport | Grenze zu Kenia
Picha: Veronica Natalis/DW

Wafanyabiashara wanaozunguka eneo la mpaka huo wameziomba serikali za nchi hizo mbili kuumaliza mgogoro huo kwani wanaoathirika ni wao.

Madereva wa malori makubwa ya kubeba mahindi wapo katika foleni kwa takribani siku nne sasa tangu serikali ya Kenya itangaze marufuku ya kupitishwa kwa mahindi yanayotoka Tanzania na Uganda kuingia katika nchi hiyo. Madereva wanalalamikia hali ngumu ya maisha katika mpaka huo wa Namanga kwani hata pesa zote za matumizi walizokuwa nazo zimekwisha na hawajui mgogoro huo utaisha lini.

Kenya imepiga marufuku ununuzi wa mahindi kutoka mataifa jirani ya Tanzania na Uganda kutokana na kile kinachoelezwa kwamba mahindi kutoka nchi hizo mbili sio salama kwa matumizi ya binadamu.

Tansania Arusha | Mais Transport | Grenze zu Kenia
Malori yaliyobeba mahindi yakiwa katika msururu mrefu katika mpaka wa Namanga upande wa TanzaniaPicha: Veronica Natalis/DW

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kilimo na chakula wa nchini Kenya inaeleza kuwa mahindi hayo yana kiwango kikubwa cha sumu kuvu, ambayo ni hatari kwa usalama wa walaji.

Corona: Changamoto za madereva wa malori mpakani Namanga

Serikali ya Tanzania hata hivyo imesema kuwa ipo katika mazungumzo na nchi ya Kenya kuhusiana na mgogoro huo japo inasema Kenya haikufuata utaratibu unaotakiwa kuzuia mahindi hayo, kulingana na naibu waziri wa kilimo nchini Tanzania Husein Bashe.

Baadhi ya wafanyabiashara wanaouzunguka mpaka huo katika wilaya ya Longido upande wa kaskazini mwa Tanzania wamezitaka serikali zote mbili kumaliza mvutano huo kwani waathirika wakubwa ni wao.

Dr. Hassan Abbas msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Siku ya Jumatatu alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa mahindi ya Tanzania bado yanaingia Kenya kupitia mipaka mingine isipokuwa mpaka wa Namanga.

Mataifa haya jirani yamekuwa katika biashara ya mazao ya chakula kwa kipindi kirefu. Mahindi, parachichi na chai ni miongoni mwa mazao ambayo Tanzania inayauza nchini Kenya.