1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kisiasa yafikiwa Guinea

Josephat Nyiro Charo22 Januari 2010

Upinzani wayapongeza makubaliano

https://p.dw.com/p/Ldbn
Jenerali Sekouba KonatePicha: AP

Mpango unaonuiwa kuleta utulivu wa kisiasa nchini Guinea umefikiwa. Jenerali Sekouba Konate, kiongozi wa utawala wa kijeshi tangu jaribio la kutaka kumuua kapteni Dadis Camara kufanyika mnamo mwezi Desemba mwaka jana, amerejea nchini Guinea akitokea Burkina Faso ambako alikwenda kuhudhuria mikutano iliyozungumzia mzozo wa kisiasa nchini Guinea. Mikutano hiyo imezaa matunda kwani makubaliano yamepatika yatakayoiongoza Guinea kurejea katika utawala wa kidemokrasia na kikatiba.

Makubiano ya Ouagadougou yamezusha matumaini miongoni mwa raia wengi wa Guinea lakini baadhi ya viongozi mashuhuri nchini humo wana shaka shaka. Jenerali Konate alirejea mjini Conakry Guinea siku ya Jumanne wiki hii baada ya kukaa wiki nzima mjini Ouagadougou nchini Burkina Faso. Akiwa mjini humo jenerali Konate alikutana na kapteni Dadis Camara na rais wa Burkina Faso Blaise Compaoré na kutayarisha makubaliano ya kisiasa yatakayoisadia Guinea kurejea katika utawala wa kiraia.

Mkataba huo uliosainiwa mnamo Januari 15 mwaka huu unataka uchaguzi ufanyike katika kipindi cha miezi sita ijayo na kumtaka kapteni Dadis Camara anayeendelea kuuguza majeraha, asijihusishe na siasa. Kwa mujibu wa mkataba huo hakuna afisa yeyote wa utawala wa kijeshi au yeyote anayetumikia jeshi la Guinea anayeruhusiwa kugombea katika uchaguzi.

Guinea Moussa Dadis Camara in Conakry Flash-Galerie
Kapteni Moussa "Dadis" CamaraPicha: AP

Makubaliano hayo yanazungumzia karibu malalamiko yote yaliyotolewa na muungano wa vyama vya upinzani, vyama vya wafanyakazi na jumuiya za kiraia, ikiwa ni pamoja na kuteuliwa kwa mwanachama mmoja wa muungano huo, Jean Marie Doré, kuwa waziri mkuu atakayeiongoza serikali ya mpito yenye wanachama 101.

Pendekezo pekee kubwa la muungano huo ambalo halikujumulishwa kwenye makubaliano ya Ouagadougou ni kuvunjwa kwa kamati ya kijeshi inayoitawala Guinea. Alpha Conde na Cellou Dalein Diallo, viongozi wa vyama viwili vikubwa vya upinzani nchini Guinea, wameyapongeza makubaliano hayo wakitumai yatachangia katika kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki. Lakini waziri mkuu mteule Jean Marie Doré, ambaye uteuzi wake hauungwi mkono na upinzani, ameonya kunahitajika mashauriano kabla serikali ya mpito kuundwa.

Mchambuzi wa maswala ya kisiasa nchini Guinea, Madani Dia, anasema licha ya makubaliano ya Ougadougou, matatizo msingi yangalipo. Anasema itakuwa vigumu kwa waziri mkuu Jean Marie Doré kuushawishi muungano wa upinzani na kamati ya kijeshi kumuunga mkono kufanikisha mabadiliko ya kiutawala nchini Guinea. Baadhi ya maafisa wa jeshi hawataki mzozo huo wa kisiasa umalizike, hali ambayo huenda ikaikwamisha mipango ya waziri mkuu kulifanyia mageuzi jeshi la Guinea.

Licha ya upinzani kuelezea wasiwasi wake kuhusiana na maswala ya kisiasa yanavyoendeshwa nchini Guinea, raia wengi nchini humo wamebaki na tumaini kwamba hali itarejea kuwa ya kawaida kadri siku zinavyopita.

Mwandishi: Josephat Charo/IPS

Mhariri: Othman Miraji