1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yashuhudiwa Kenya na Afrika Kusini

20 Machi 2023

Maandamano yameshuhudiwa nchini Kenya. Polisi wa Nairobi walirusha mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya waandamanaji. Nchini Afrika Kusini, polisi wametumwa sehemu mbalimbali huku maandamano makubwa yakitarajiwa leo.

https://p.dw.com/p/4OvXO
Kenia l Proteste in Nairobi l Ausschreitungen im Slum von Nairoby
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Maandamano hayo ni ya kupinga gharama ya juu ya maisha na madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa mwaka jana nchini Kenya. Takribani watu 22 wamekamatwa, wakiwemo wabunge wawili wa upinzani.

Raila Odinga, mpinzani nchini Kenya na aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais mwezi Agosti mwaka jana ameitisha maandamano ya nchi nzima akijaribu kutumia hisia inayoongezeka ya raia wa nchi hiyo kutoridhishwa na uongozi wa William Ruto. Odinga ametoa wito wa kuandamana kutoka wilaya kuu ya kibiashara kuelekea Ikulu ya Rais ili kurejesha kile walichokitaja kuwa "ushindi ulioporwa."

Miongoni mwa wanaochukizwa na uongozi wa sasa ni pamoja na baadhi ya waliompigia kura Ruto ambao wanahisi hajatekeleza ahadi yake ya kuwasaidia wale waliosahaulika nchini humo na wanaoitwa "wapambanaji", au Wakenya wa tabaka la wafanyikazi.

Kenia l Proteste in Nairobi l Ausschreitungen mit der Polizei
Polisi mjini Nairobi wakikabiliana na mwandamanaji 20.03.2023Picha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kujihami na waliokuwa na vifaa vya kutuliza ghasia, waliwarushia mabomu ya machozi mamia ya waandamanaji ambao nao walirusha mawe katika mtaa duni wa Kibera huku wakiimba: "Ruto lazima aondoke."

Soma pia: Polisi Kenya yawatawanya waandamanaji wa upinzani

Licha ya ahadi za Ruto za kupunguza gharama za maisha tangu alipochukua mamlaka mwezi Septemba mwaka jana, mfumuko wa bei umeendelea kuwa juu katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwezi Februari, mfumuko wa bei ulipanda hadi 9.2% kwa mwaka kutoka 9.0% ukilinganisha na mwezi uliopita, licha ya kuwa ni kiwango cha chini kuliko matokeo ya mwezi Oktoba ambapo mfumuko wa bei ulifikia 9.6%.

Odinga alipinga matokeo ya uchaguzi katika Mahakama ya Juu mwaka jana, lakini Mahakama hiyo ilithibitisha ushindi wa Ruto na kulishuhudiwa matukio machache ya vurugu ambayo yalitia doa uchaguzi wa mwaka 2007 na 2017.

Maandamano yatarajiwa pia Afrika Kusini 

Polisi wametumwa sehemu mbalimbali nchini humo baada ya chama cha mrengo wa kushoto kutoa wito wa maandamano ya kitaifa. Kumekuwa na hofu ya kushuhudiwa kwa mara nyingine machafuko ambayo yalisababisha vifo miaka miwili iliyopita.

Ulinzi umeimarishwa katika Majengo ya Umma na makao makuu ya serikali mjini Pretoria, ambapo waandamanaji wanatarajiwa kuandamana baadaye leo. Chama cha tatu kwa ukubwa nchini humo cha Economic Freedom Fighters (EFF), kimewataka raia wa Afrika Kusini kuingia mitaani na kusitisha shughuli za nchi hiyo.

Vergewaltigungen erschüttern Südafrika
Afrika ya Kusini hushuhudia maandamano yenye vurugu kubwa. Pichani, ni Mwanamume akiwa ameshika panga wakati wa maandamano ya kuwasaka wachimbaji haramu maarufu kama "Zama-Zama" huko West Rand 08.08.2022.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Mamlaka zimetaja kuwa katika hali ya tahadhari ili kuzuia na kupambana na vitendo vyovyote vya uhalifu na kudumisha utulivu wa umma. Bunge limetangaza kuwa Rais Cyril Ramaphosa ameidhinisha kutumwa kwa wanajeshi 3,474 kuwasaidia polisi katika kudhibiti maandamano hayo.

Soma pia:Afrika Kusini: Wanajeshi 25,000 wahitajika kudhibiti ghasia 

Takriban waandamanaji 87 walikamatwa kwa makosa yanayohusiana na ghasia usiku wa kuamkia leo. Barabara za Pretoria na Johannesburg zilikuwa kimya asubuhi ya Jumatatu, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa. Magari machache yameonekana kipita katika mitaa ambayo kwa kawaida huwa na shughuli nyingi.

Wito huo wa maandamano umeibua kumbukumbu za ghasia mbaya za Julai mwaka 2021, kulipotokea ghasia mbaya zaidi kushuhudiwa tangu mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, ambapo watu wasiopungua 350 waliuawa katika maandamano yaliyochochewa na kitendo cha kufungwa kwa rais wa zamani Jacob Zuma na kusababisha ghasia na uporaji. Ramaphosa ameagiza vyombo vya sheria kuhakikisha hakuna marudio ya machafuko ya mwaka 2021.