1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashahidi wawili wa mwisho kusikilizwa na bunge

21 Novemba 2019

Kamati ya bunge inayosikiliza ushahidi katika mchakato wa kumshitaki rais Donald Trump wa Marekani, hii leo watawasikiliza mashuhuda wawili wa mwisho katika mchakato huo unaorushwa moja kwa moja hadharani.

https://p.dw.com/p/3TRcd
USA Zeuge untermauert Vorwürfe gegen Trump in Impeachment-Ermittlungen
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Wachunguzi kwenye mchakato wa bunge wa kumshitaki rais wa Marekani Donald Trump hii leo watasikiliza ushahidi kutoka kwa mashahidi  wawili muhimu ambao wanadai waliingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu namna rais Trump pamoja na watumishi wengine kwenye ofisi ya rais ya Oval walivyokuwa wakiitekeleza sera ya mambo ya nje nchini Ukraine. 

Mshauri wa masuala ya siasa katika ubalozi wa Marekani nchini Ukraine David Holmes amesema alikuwa akipata chakula cha mchana na balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Ulaya, Gordon Sondland majira ya joto ya mwaka huu wakati alipomsikia rais Trump aliyekuwa akizungumza na simu akiomba ujumbe kwa ajili ya uchunguzi aliomtaka rais wa Ukraine kuufanya. Kulingana na Holmes katika ushahidi wa faragha alioutoa mapema, mazungumzo hayo yalikuwa ya furaha mno, kiasi ambacho hakuwahi kushuhudia.

Shahidi mwingine Fiona Hill amesema mkuu wake wa baraza la usalama wa taifa John Bolton, alikatisha mkutano na maafisa wa Ukraine walipotembelea ikulu ya White House, wakati Sondland alipoanza kuwauliza kuhusu kile alichokitaja kuwa ni "chunguzi". Mashahidi hao wawili wanaotarajiwa kutoa ushahidi hii leo, ni wa mwisho kusikilizwa kwenye mchakato huo wa uchunguzi unaorushwa moja kwa moja hadharani kupitia televisheni.

USA Impeachment öffentliche Anhörung
Kamati inayosikiliza ushahidi wa uchunguzi wa kumshitaki rais Donald Trump ikiwa inaendelea kuwasikiliza mashahidPicha: AFP/S. Loeb

Hapo jana, balozi Sondland alipotoa ushahidi wake mbele ya wachunguzi alisema alielekezwa na rais Trump kushirikiana na wakili wake binafsi Rudy Giuliani kuishinikiza Ukraine. Sondland amesema katika hotuba aliyoiandaa kabla kwamba, Giuliani alitaka kumshinikiza rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy kuchunguza uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016 pamoja na mtoto wa kiume wa makamu wa rais na mpinzani mkubwa  kwenye uchaguzi wa 2020, Joe Biden.

Aidha, balozi Sondland aliiambia kamati hiyo ya bunge ya uchunguzi kwamba waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu katika serikali ya Trump walikuwa wakiarifiwa kuhusu majadiliano hayo ya Ukraine. Alisema alimuelezea wasiwasi wake makamu wa rais Mike Pence kwamba kusimamishwa kwa msaada wa kijeshi wa Marekani nchini Ukraine kulikuwa na mahusiano na uchunguzi ambao Trump ameuomba.

USA | Mike Pompeo | Israel Siedlungsbau legal
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompe atajwa kwenye uchunguziPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/A. Harnik

Akiwa mjini Brussels, Pompeo alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na uchunguzi huo na namna anavyohusishwa katika ushahidi uliotolewa na balozi Sondland, aliwaambia kwamba pamoja na mengine lakini anajivunia sana mafanikio yaliyofikiwa nchini Ukraine kupitia sera ya Marekani kuelekea Ukraine.  

"Sijaangalia ushahidi. Sitajiondoa kwenye suala hili. Ninajua kabisa sera ya Marekani ilikuwa na uhusiano gani na Ukraine nilikuwa ninaifanyia kazi na ninajivunia sana yale ambayo tumeyatimiza."alisema Pompeo.

Kulingana na balozi Sondland, haikuwa siri kwamba ilikuwa ni kama kurejesha fadhila kwa Ukraine, na kwa maneno mengine, ni kwamba rais wa Ukraine angeweza kualikwa kutembelea White House, kama shukrani ya kuanzisha uchunguzi dhidi ya Biden.

Matamshi hayo yanapingana na yale ya Trump kwamba hakukuwa na aina yoyote ya kurejesheana fadhila kati ya mataifa hayo.

Kwenye uchunguzi huo, Sondland alikiri kwamba hakuwahi kuzungumza moja kwa moja na Trump kuhusu msaada wa kijeshi nchini Ukraine kuwa ni sehemu ya masharti ya uchunguzi wa kisiasa. Na badala yake alisema hiyo ilikuwa ni fikra yake binafsi iliyotokana na matamshi ya Giuliani