Kumbukumbu ya mauaji ya Bucha, miaka minne baadaye
31 Machi 2026
Mawaziri kadhaa wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wakiongozwa na mwanadiplomasia Mkuu wa umoja huo Kaja Kallas, wamehudhuria kumbukumbu ya miaka minne tangu mauaji ya watu wengi katika mji wa Bucha Ukraine. Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na Urusi ilipoivamia Ukraine.
Kwenye taarifa ya pamoja kwenye kumbukumbu ya miaka minne tangu mauaji ya Bucha yalipofanyika, mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya wamekariri nia yao ya kutetea uhuru wa Ukraine
Mawaziri hao wameeleza kile walichokiita kuwa "dhamira yao isiyoyumba ya kuhakikisha uwajibikaji kamili wa Shirikisho la Urusi, kwa ukiukaji wowote wa sheria za kimataifa nchini au dhidi ya Ukraine".
Msukumo wa Urusi kuwajibishwa kisheria kwa maafa ya Bucha
Akiwa njiani kuelekea Kyiv, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wale waliotoa amri za kuua katika maeneo kama Bucha wanawajibishwa, sawa na wale waliofanya ukatili huo. Umoja wa Ulaya unataka maafa hayo yachunguzwe ili wahusika wawajibishwe kisheria. Vinginevyo, Kallas amesema kunaweza kuwa na kulipizana kisasi.
"Pia ni muhimu kuweka suala la uwajibikaji mezani. Kwa sababu bila uwajibikaji, ikiwa makosa hayo hayatadhibiwa, basi hakuna uwezekano wa kuwa na haki na amani ya kudumu, kwa sababu haki ni sehemu ya mchakato wa amani,” amesema Kallas.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul aliyekuwa miongoni mwa waliohudhuria kumbukumbu hiyo amesema, mauaji ya Bucha yanasalia kama kidonda kisichopona kwa Waukraine na Ulaya nzima.
Akizungumza katika mji mkuu wa Ukraine, Wadephul alisema Bucha inawakilisha "makosa yaliyokusudiwa dhidi ya raia, na ni sehemu muhimu ya vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Mzozo wa Ukraine umesahaulika kwa sababu ya mzozo wa Iran?
Huku juhudi zinazoongozwa na Marekani za kumaliza vita zikiwa zimesimama na Washington ikiupa mzozo wa Mashariki ya Kati kipaumbele, serikali za Ulaya zinataka kuendelea kuangazia vita hivyo vya Ukraine ambavyo kwa miongo mingi, ndivyo vikubwa zaidi barani humo na sasa viko katika mwaka wa tano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha amesema uwepo wa wawakilishi wa Umoja wa Ulaya ni ishara kwamba Urusi haitakwepa kuwajibishwa na haki kwa wahanga itatimia.
Kulingana na maafisa wa Ukraine na pia mashirika ya kutetea haki za binadamu, vikosi vya Urusi viliwaua zaidi ya watu 400 katika mji mdogo wa Bucha nchini Ukraine.
Ukraine yashambulia vituo vya mafuta vya Urusi
Wakati hayo yakijiri, droni za masafa marefu za Ukraine zilisambaratisha vituo vya mafuta vya Urusi katika Bahari ya Baltiki usiku wa Jumatatu kwa mara ya tano katika kipindi cha zaidi ya wiki moja.
Mashambulizi hayo ni juhudi za Kyiv kujaribu kuzuia Moscow isipate faida kutokana na mauzo yake ya mafuta katikati ya mgogoro wa nishati uliosababishwa na vita vya Iran.
Marekani ililegeza vikwazo vyake dhidi ya mafuta vya Urusina kuruhusu iuzwe mnamo wakati uhaba wa mafuta umechochewa na mkwamo katika mlango wa bahari wa Hormuz.
(DPAE, EBU,RTRE)